Tunalaani vikali mauaji ya watafiti

04Oct 2016
Mhariri
Nipashe
Tunalaani vikali mauaji ya watafiti

JANA vyombo mbalimbali vya habari viriripoti tukio la kusikitisha la mauaji ya watafiti wawili na dereva mmoja wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian (SARI) jijini Arusha, kisha miili yao kuchomwa moto katika Kijiji cha Iringa Mvumi wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma.

Watafiti hao waliuawa kimyama wakati wakifanya utafiti wa udongo, baada ya baadhi ya wanakijiji kusambaza taarifa za uvumi kuwa watafiti hao ni wanyonya damu.

Waliouawa wametajwa kuwa ni Nicas Magazine, aliyekuwa dereva wa gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin na watafiti wawili ambao ni Teddy Lumanga na Jaffari Mafuru.

Mauaji hayo yalitokea Jumamosi katika kijiji cha kijiji hicho, baada ya watu hao waliokuwamo katika gari kuvamiwa na wanakijiji na kuwakatakata kwa mapanga pamoja na silaha za jadi kisha kuwachoma moto hadi kufa.

Taarifa zinaeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni baadhi ya mwanamke mmoja kupiga yowe kuwafahamisha wanakijiji kuwa ameona watu wanaohisi kuwa ni wanyonya damu.

Habari hizo zinasema kuwa baada ya taarifa hizo kufika kijijini, mchungaji wa madhehebu ya Kanisa la Christian Family alikitangazia kijiji kupitia kipaza sauti cha kanisani kuwa wamevamiwa na wanyonya damu ndipo wanakijiji walipokwenda na kufanya kitendo hicho cha kikatili.

Tunalaani vikali kitendo hicho cha ukatili dhidi ya ubinadamu na tunawapa pole familia, ndugu, jamaa na wafanyakazi wa SARI ambao wamewapoteza wapendwa wao waliokuwa kazini wakitekeleza majukumu yao.

Tukio hilo linaonyesha ni jinsi gani wananchi wengi wanavyopuuza maelekezo na elimu ambavyo wamekuwa wakipewa mara kwa mara kuhakikisha kwamba wanajiepusha na tabia ya kujichukulia sheria mikononi.

Hapakuwapo na umuhimu wowote wa kuwashambulia kwa silaha kisha kuwaua. Kama walihisi kuwa watafiti hao sio raia wema, walipaswa kushirikiana kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vinavyohusika.

Tabia ya kujichukulia sheria mikononi matokeo yake ni kuwa vinawaathiri watu wasio na hatia kama ilivyotokea katika tukio hilo la Dodoma, ndiyo maana kuna mahakama ambayo nayo huamua kesi baada ya kupata ushahidi usioacha shaka yoyote.

Inashangaza na kusikitisha kuona baadhi ya watu katika jamii wakiendelea kuamini na kukumbatia imani potofu na zilizopitwa na wakati zikiwamo za ushirikina na kuwapo na watu wanaonyonya damu (mumiani).

Ni imani hizi ambazo zimekuwa zikisababisha mauaji ya watu wasio na hatia katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu hususani wazee, vikongwe na watu wengine wanaotuhumiwa bila ushahidi kuwa ni wachawi.

Aidha, ni jambo linaloshangaza kuwasikia baadhi ya watu wanaojiita viongozi wa dini kushiriki kuwahamasisha wananchi kujichukulia sheria mikononi dhidi ya watu wanaozushiwa tuhuma ambazo hazijathibitika kuwa za kweli.

Kwa kuwa viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa kwa jamii, wanapaswa kutimiza wajibu wao wa kuhubiri amani, upendo na maridhiano badala ya kuwaelekeza waumini wao kufanya vitendo vya chuki na uhalifu.

Ni matarajio yetu kwamba wote waliohusika kufanya kitendo hicho cha kinyama watakamatwa na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Tunaamini kuwa hilo litatekelezwa kufuatia kauli ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, kuwa hadi Jumapili watu 30 walikuwa wakishikiliwa, na ya Mkuu wa mkoa huo, Jordan Rugimbana, kuwa wahusika wote watasakwa na kutiwa mbaroni.

Habari Kubwa