Tunamngoja nani kunusuru Kariakoo?

20Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tunamngoja nani kunusuru Kariakoo?

BUNGE limeambiwa kwa kina jinsi ambavyo Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam lilivyo taabani, likihesabu siku za  kuishi kutokana na kukimbiwa na wateja. Chanzo cha kuachwa na wanunuzi hasa kutoka nchi jirani za Uganda, Zambia, Kongo na Malawi ni ugumu wa biashara unaochangiwa na kodi.

Historia ya soko la Kariakoo inaelezwa kuwa ilianzia wakati wa ukoloni wa Mjerumani na kwamba kiwanja lilipo soko hilo leo, ndiyo yaliyokuwa yawe makao makuu ya ofisi ya Utawala wa Serikali ya Ujerumani.

Lakini, mpango huo ulitibuliwa na Waingereza baada ya kuwashinda  kwenye Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia.

Ni baada ya Wajerumani kushindwa na Waingereza kulichukua koloni lao la Tanganyika, hatua iliyoibadilisha Kariakoo kutoka kuwa  makao makuu ya Mjerumani kuwa kambi ya wanajeshi wa kubeba mizigo kwa ajili ya askari wa  Kiingereza, iliyokuwa ikijulikana kama Carrier Corps.

Hiyo ndiyo asili ya soko la Kariakoo linaloonekana leo. Kwa ujumla ni kitega uchumi ambacho serikali ilikianzisha miaka ya 1970, kazi iliyofanywa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo iliagizwa kujenga soko la kisasa na  kuwapatia Watanzania mahitaji ya chakula, mavazi na bidhaa nyingine za aina zote tena likitakiwa kuwahudumia wananchi kwa miaka zaidi ya 50.

Soko hili ni mojawapo ya vivutio, alama ya utambulisho na pambo la jiji la Dar es Salaam pengine na Afrika.

Soko la Kariakoo na jingine liitwalo Markatu lilipo Addis Ababa Ethiopia, ni miongoni mwa masoko makubwa na ya kipekee barani Afrika.

Hivyo, Kariakoo si kitega uchumi cha kuupuzwa. Ni jambo la kuhuzunisha pale bunge linavyoelezwa kuwa soko hilo lipo kwenye hati hati, kutokana na ugumu wa biashara.

Kitovu hicho cha biashara ambacho zamani kilikuwa kimbilio la wafanyabiashara wa Zambia, Malawi, Uganda na Congo siku hizi kinaporomoka.

Sababu zimetajwa bungeni kuwa ni pamoja na utitiri wa kodi unaotozwa kwenye bidhaa unaozifanya kuwa ghali zaidi na kuwakimbiza wateja hasa kutoka mataifa ya jirani.

Huu si wakati wa kulaumiana bali ni muda wa kutafuta ufumbuzi ili kuifanya Kariakoo izidi kung’ara na kuongeza mapato ya jiji la Dar es Salaam pamoja na serikali kuu.

Serikali ina wataalamu na wabobezi wa masuala ya biashara na namna ya kuweka mikakati ya kuvutia wateja hasa kwenye maeneo hayo.

Tunawashauri kufanya mbinu na kubuni mikakati mbalimbali itakayoliwezesha soko hilo kuwa na viwango vya juu na bora hata kuliko ilivyokuwa hapo zamani.

Pengine ni wakati wa kuweka eneo ama ukanda maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara kutoka nchi jirani . Eneo litakalokuwa na upendeleo maalumu.

Ikumbukwe hizi ni zama za ushindani, ukienda Kenya lipo soko la Eastleigh husoma ‘Islii’ ambalo ni maarufu kwa bidhaa za aina mbalimbali zinazopatikana Kariakoo na linalovutia wateja kutoka sehemu nyingi za kusini na mashariki mwa Afrika.

Hivyo ni wakati wa kujua kuwa kuna ushindani, lakini Tanzania tofauti na mataifa mengine ya ukanda huu ni eneo lenye usalama mkubwa na aamani.

Hizo ni baadhi ya sifa zinazoifanya bandari ya Dar na soko la Kariakoo kuwa kwenye chati kila wakati.

Hima serikali, mamlaka za kodi, viongozi na wadau kwenye biashara chondechonde imarisheni Kariakoo na kuirudishia hadhi iliyokuwa nayo.

Habari Kubwa