Tunasubiri utekelezaji agizo la Simbachawene

22Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tunasubiri utekelezaji agizo la Simbachawene

JANA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alipiga marufuku kuingia na silaha kwenye maeneo ya starehe kama baa, kambi za muziki, harusi na mengine kwenye mikusanyiko ya watu.

Aidha, alisema ni lazima kuwapo utaratibu wa wahusika na maeneo hayo kufanya ukaguzi mlangoni kabla ya watu kuingia ndani.
 
Agizo la Waziri huyo limekuja siku chache, baada ya kutokea tukio la Alex Koroso (37), kummiminia risasi sita Gifti Mushi, na kumuua kisha naye alijiua kwa kujipiga risasi wakiwa kwenye baa ya Lemax, Sinza Dar es Salaam.
 
Baada ya tukio hilo kulikuwa na mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii, juu ya namna wanaomiliki silaha wako huru  kwenda nazo kila mahali na hakuna utaratibu wa kukagua na hata kama ukaguzi unafaponyika, siyo wa kuhakikisha usalama.
 
Mathalani, tukio la Alex alianza kufanya vurugu tangu asubuhi kwa kuwa alifika kwenye baa hiyo akiwa ametoka kukesha kwenye baa nyingine, aliendelea kunywa na kuna wakati alimwaga risasi mezani na moja kuanguka chini ikaokotwa na msimamizi wa baa hiyo lakini  aliendelea na starehe zake.
 
Tunaipongeza serikali kwa uamuzi huu na, ni jambo jema, lakini tunapenda kutahadharisha kuwa isiwe ni zimamoto kwa kuwa kuna tukio limetolea bali iwe ni utaratibu endelevu na ufuatiliwe.
 
Lakini bado kuna maswali mengi kwa kuwa zipo baa ambazo ni za wazi hazina mlango mmoja maalum wa kuingilia, bali unaweza kuingia kokote na kukaa ukahudumiwa, je, hili nalo litafanyikaje katika kudhibiti?
 
Pia, kuna baa zinazoanzishwa kwenye maduka ya vinjwaji kwa kuweka viti kadhaa nje kwa ajili ya watu kupata kinywaji, nako hakuna uratatibu wa kukagua.
 
Hakuna ubishi kwamba ukaguzi haufanyiki kuanzia kwenye kumbi za sherehe na baa, kwa kuwa watu hujiingilia tu, lakini yapo maeneo ambayo ukaguzi haufanyiki ipasavyo bali walinzi wanaruhusu watu kupita kuendelea na shughuli zao, na hili lipo katika moja ya eneo maarufu la manunuzi na matembezi (jina linahifadhiwa).
 
Waziri kutoa agizo ni jambo moja, utekelezaji ni jingine, ni muhimu ukatolewa utaratibu wa namna ya kufunga vifaa maalum vya ukaguzi na kufuatilia utekelezaji mara kwa mara, kwa kuwa inawezekana kufanyika kwa muda mfupi baada ya hali kutulia maisha yakaendelea.
 
Kama vifaa hivi vitafungwa, ni muhimu kufuatilia usalama wake, lakini kutoa elimu kwa wamiliki kuwa wanapoona hali ya kutoweka kwa amani wasiangalie uwezo wa mteja au fedha atakazolipa, bali usalama wa waliopo kwenye eneo hilo.
 
Tukio la Alex limeacha funzo kwa wamiliki na wasimamizi wa baa kuwa wanapaswa kuhakikisha usalama wa wateja wao, kwamba kama mtu anaonyesha lolote la kuvunja amani, hatua zichukuliwe mapema.
 
Pamoja na uamuzi huo, ni muhimu kupima afya ya akili ya watu wanaomiliki silaha hizo, kwa kuwa yaliyokuwa yanaendelea kwenye baa hiyo yalionyesha siyo kwamba mtendaji alikuwa amelewa tu, bali kulikuwa na tatizo jingine kubwa.
 
Ni muhimu kupitia kila mara umiliki wa silaha kama wahusika wanafuata taratibu, kwa kuwa baada ya tukio hili imetokea mifano mingi inayoeleza kuwa wapo watu hutumia kutishia watu au kuonyesha kuwa wanazimiliki, jambo ambalo halitakiwi kuwa huko.
 
Agizo la waziri lina nia njema kabisa, ila bado tunasisitizo kuwe na utekelezaji isije ikawa ni zimamoto kwa kuwa kuna tukio limetokea na kusababisha majadala kwenye mitandao ya kijamii.
 

Habari Kubwa