Tunataka Spika atakayesimamia majukumu ya Watanzania

20Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tunataka Spika atakayesimamia majukumu ya Watanzania

WIKI hii ndiyo uamuzi wa majina matatu yatakayopelekwa kwenye kikao cha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kupigiwa kura ikiwa ni baada ya kumalizika mchujo ngazi ya Sekretarieti na Kamati Kuu ya CCM.

Ndani ya chama hicho jumla ya makada 70 ambao baadhi wamewahi kuwa au ni viongozi hadi sasa katika nafasi mbalimbali, walijitokeza kuomba ridhaa ya chama chao kugombea kiti cha Spika wa Bunge.

Kati ya vyama vya siasa 22 vilivyoko nchini kwa sasa, ni ADC pekee ndiyo kimesimamisha mgombea, Maimuna Kassim.

Mkutano wa sita wa Bunge la 12, utafanyika kuanzia Februari mosi hadi 11, mwaka huu, ukijumuisha wabunge 392 ikiwa ni 263 wa majimbo, 113 viti maalum, watano kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wabunge wa Kuteuliwa na Rais 10.

Hadi sasa mchuano mkali uko ndani ya CCM kwa kuwa kina wabunge 363, ikiwa ni 213 wa majimbo, Viti Maalum Bara na Visiwani 112, wa kuteuliwa tisa, hivyo kwa wingi wa kura spika atatokana na chama hicho.

Kwa mujibu wa kitabu cha orodha ya wabunge kilichoko kwenye tovuti ya Bunge, wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni 20 kati yake mmoja wa jimbo na 19 Viti Maalum.

Aidha, ACT-Wazalendo kina wabunge wa majimbo wanne na Chama cha Wananchi (CUF) kina wabunge watatu.

Watanzania wana matarajio makubwa kwa Spika atakayepatikana kuongoza muhimili huo utoe sura ya uwakilishi wa wananchi wa kawaida ambao walishiriki kupiga kura kwenye uchaguzi wa 2020.

Kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Tanzania inasema, Bunge litakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano, ambacho kitakuwa na madaraka kwa niaba ya wananchi ya kusimamia na kuishauri Serikali ya Muungano pamoja na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake.

Katiba ambayo ndiyo sheria mama inalitaja Bunge kama chombo cha uwakilishi wa wananchi kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka ya Bunge linawenza kumuuliza waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma.

Pia kujadili utekelezaji wa kila wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti, kujadili na kuridhia mpango wowote wa muda mrefu au muda mfupi unaokusudia kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo.

Mjukumu mengine ni kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo, kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu nchi ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.

Tunataraji spika atakayepatikana ataweka kipaumbele kwenye kusimamia majukumu yake ili tuone uwakilishi wa wananchi kwenye chombo hicho.

Tupo kwenye ulimwengu wa kidigitali ambao wananchi wanapata taarifa kwa haraka zaidi, wanahitaji kujua wanachojadili, yanayopitishwa na uwajibikaji wa chombo chao, hivyo lazima tupate spika anayejua mabadiliko yaliyoko duniani na mahitaji ya wananchi kwa sasa.

Tunapokumbuka maspika waliopita hasa wakati wa mfumo wa vyama vingi Bunge linalokumbukwa ni la Tisa lililoongozwa na marehemu Samuel Sitta, ambalo lilijulikana kama Bunge la speed (kasi) and standard viwango.

Katika Bunge hilo tuliona wabunge wakihoji serikali mambo ya msingi yanayogusa maisha ya watu, kushughulikia rushwa ikiwamo kuunda kamati ya kuchunguza sakata la rushwa ambalo lilipelekea baadhi ya viongozi kuwajibika.

Tunaamini spika akiwa imara, mwadilifu na mwajibikaji tutakuwa na Bunge imara ambalo litafuatilia kwa karibu utekelezaji wa shughuli za serikali pamoja na kutunga sheria zinazoendana na wakati wa sasa na uhalisia wa maisha.

Habari Kubwa