Tunatarajia kasi uunganishaji umeme

07Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tunatarajia kasi uunganishaji umeme

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limetangaza kurudisha gharama za awali za kuunganisha huduma ya umeme kwa wateja wake, kama zilivyokuwa zimetangazwa kwenye gazeti la serikali mwaka jana.

Gharama hizo zilitangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA), kwenye gazeti la serikali namba 1020 Desemba 4, mwaka jana, na imefafanuliwa kuwa gharama zote zimejumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa gharama hizo ziliidhinishwa rasmi na EWURA Novemba 25, mwaka jana, baada ya kupitia mchakato wa tathmini wa bei kulingana na gharama halisi ya vifaa vya uunganishaji umeme na kwamba kwa sasa itaondoa kero ya kushindwa kuwafungia huduma ya umeme wateja wake kwa wakati.

Kuanzia sasa gharama za kuunganisha umeme mjini ndani ya mita 30 kwa mteja wa njia moja kutoka kwenye miundombinu ya umeme ni Sh. 320,960, kwa mteja wa njia moja ndani ya mita 70 kutoka kwenye miundombinu ya umeme ni Sh. 515,618 na kwa umbali wa njia moja ndani ya mita 120 kutoka kwenye miundombinu ya umeme ni Sh. 696,670.

Pia gharama za kuunganisha umeme mjini ndani ya mita 30 kwa mteja wa njia tatu kutoka kwenye miundombinu ya umeme ni Sh. 912,014, kwa mteja wa njia tatu ndani ya mita 70 kutoka kwenye miundombinu ya umeme ni Sh.
1,249,385, umbali wa njia tatu ndani ya mita 120 kutoka kwenye miundombinu ya umeme ni Sh. 1,639,156.

TANESCO imesema gharama ya kuunganisha umeme vijijini kwa wateja wa njia moja ni Sh. 27,000 kama ilivyoelekezwa na EWURA.

Pia wateja waliokwisha lipia Sh. 27,000 kwa ajili ya kuunganishiwa huduma hiyo, wanatakiwa kufika ofisi za shirika hilo.

TANESCO ilipata nguvu ya kutekeleza bei hizo baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kusema wazi kuwa bei ya kuunganishia watu umeme kwa sasa haina uhalisia, kiasi cha wengi kushindwa kupata huduma hiyo.

Alisema bayana kuwa gharama hizo ndogo zilisababisha shirika hilo kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kuunganishia watu umeme, na kuagiza wasiweke viwango vya juu sana bali halisia.

Katika hili kuna jambo kubwa la kujifunza kwamba wakati mwingine watendaji wanashindwa kushauri au kusema uhalisia wa uendeshaji kwa kuwa kiongozi mkuu ndiye aliyeamua, matokeo yake mashirika yanaumia yenyewe na wananchi wanashindwa kupata huduma sahihi.

Ni muhimu viongozi wakuu wanapofanya uamuzi kabla ya kutangaza kwa umma wawe wametafakari kwa kina, ikiwamo kupokea ushauri ili kuepusha kuyaumiza mashirika na taasisi zake au kuwaweka kwenye wakati mgumu watendaji wake kama tunavyoona kwa TANESCO.

Sasa TANESCO wamepewa rungu na bei halisi zitatumika kuunganishia wananchi umeme, tunatarajia kuona kasi ya kuwahudumia wateja ambao watalipa ili kuondoa usumbufu au kukaribisha mazingira ya rushwa.

Tunatarajia kuona mabadiliko na kasi ya kuhudumia wateja ili kufungiwa umeme isiwe anasa bali haki ya Mtanzania ambaye ameshalipia huduma hiyo kwa mujibu wa sheria na sio kukwamisha hadi uwe unafahamiana na mtu au kutoa kitu kidogo.

Miaka ya nyuma kupata huduma TANESCO ilikuwa ngumu mpaka ufahamiane na mtu, ndiyo ufungiwe huduma hiyo.

Tunatarajia kuona mabadiliko makubwa hasa TANESCO mpya inayoangaza maisha ya watu badala ya kuwaumiza, hasa katika kufunga umeme, kurekebisha miundombinu, kubadili mita au kukatika katika kwa nishati hiyo bila taarifa.

Kwa sasa hakuna malalamiko ya kubambikiwa bili kutokana na mteja, kulipa kabla ya kutumia (LUKU) badala ya kusoma mita, jambo ambalo limepunguza malalamiko.

Pia ni muhimu kuboresha huduma kwa kuruhusu wawekezaji binafsi kwenye nishati mbadala hasa kuondoa vikwazo kwa wanaotaka kuwekeza kwenye umeme wa jua, upepo, joto, ardhi na maji ambao watasambaza kwa wananchi wa kawaida.

Habari Kubwa