Tunawapongeza waliosaidia madereva kurejea wakiwa hai

23Sep 2016
Mhariri
Nipashe
Tunawapongeza waliosaidia madereva kurejea wakiwa hai

WATANZANIA juzi walifurahia kurejea nchini kwa madereva 10, ambao walitekwa na kikundi cha waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) cha Mai Mai.

Madereva hao walipata mkasa huo Septemba 14, mwaka huu wakiwa miongoni mwa madereva 15, wakiwamo watano wa Kenya.

Waasi baada ya kuwateka madereva hao ambao walikuwa wamekwenda DRC kupeleka mizigo, walitoa masharti ya kutaka wapatiwe fedha taslimu Dola za Marekani 5,000 kila mmoja ili wawaachie, vinginevyo wangewaua kama kiasi hicho cha fedha kisingetolewa ndani ya saa 24.

Waliofanya kitendo hicho wamedhihirisha kwamba ni watu wakatili wasio na chembe ya ubinadamu, kwa sababu madereva hao walikuwa ni raia wema waliokwenda nchini humo kutekeleza kazi yao halali ya kujipatia kipato.

Ukatili huo ulibainishwa juzi na baadhi ya madereva waliosimulia jinsi tukio hilo lilivyotokea hadi kuokolewa kwao na wanajeshi wa Jeshi la Serikali ya DRC. Simulizi hukusiana na mateso waliyopewa na watu hao zinasikitisha.

Kilichowasaidia wasiuawe ni hatua ya haraka iliyochukuliwa na wanajeshi wa DRC kuamua kufanya msako wa haraka katika maeneo ya msituni walikokuwa wanashikiliwa.

Tukio hilo limetuachia fundisho kwamba pamoja na jumuiya ya kimataifa kuweka vitendo vya utekaji watu kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa ya uhalifu, bado kuna watu wanafanya uhalifu huo bila woga.

Uhalifu huo pamoja na ugaidi, usafirishaji wa binadamu, dawa za kulevya, uharamia na uhalifu dhidi ya ubinadamu ni makosa ambayo dunia inashirikiana kukabiliana nayo na adhabu zake ni kubwa.

Tunawapongeza wote waliofanikisha jitihada wa kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu waliorejea wakiwa hai na afya njema na kuungana na familia, jamaa, ndugu na marafiki zao, ambao walikuwa wamekata tamaa kama wangewaona tena.

Miongoni mwa wanaostahili pongezi ni Serikali za Tanzania na DRC. Jeshi la DRC pamoja na kampuni wanayofanyia kazi ya Simba Logistics Ltd kutokana na kupeana taarifa ambazo hatimaye ziliwezesha kuokolewa kwao.

Kauli aliyoitoa Balozi wa DRC nchini, Jean Pierre Mutamba, kwamba kuna haja ya kutoa taarifa pale madereva wanapokuwa wanakwenda DRC ili ubalozi huo toe taarifa kwao pamoja na kufuatilia ni suala ambao lina umuhimu mkubwa.

Tunasema hivyo kwa kuwa licha ya kuimarishwa kwa ulinzi, ikiwamo magari ya mizigo yanayokwenda nchini humo kusindikizwa na askari, bado hali ya usalama ya DRC haijatenegamaa kwa asilimia kubwa kutokana na uwapo wa makundi mengi ya waasi pamoja na wahalifu wengine.

Tunashauri kwamba kuna haja kwa serikali kuweka utaratibu wa kuwataka wasafirishaji wa mizigo kuwakatia bima maderava wao wanaokwenda katika maeneo yasiyo salama kama DRC kuwa na bima ili pale ikitokea wakapata matatizo familia zao na watu wanaowategemea waweze kusaidiwa.

Ni matarajio yetu kwamba serikali itauona umuhimu huo kwa kutilia maanani changamoto ambazo madereva wanaosafiri masafa marefu wanakumbana nazo, likiwamo tukio la kutekwa DRC.

Habari Kubwa