Tushangilie kwa amani Simba na Yanga

01Oct 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tushangilie kwa amani Simba na Yanga

LEO hisia za mashabiki wa soka nchini zinaelekezwa kwenye uwanja wa Taifa kwenye pambano la vigogo wa soka Tanzania Simba na Yanga ambazo zinaongoza kwa kugawana na idadi kubwa ya mashabiki.

Mchezo huo ni wa kwanza kuzikutanisha timu hizo kwenye msimu huu na ni matarajio ya wengi uwanja wa Taifa leo utafurika kwa idadi kubwa ya mashabiki.

Kama ilivyo miaka yote, mchezo huu umebeba hisia za mashabiki ambapo maneno ya utani kwa pande zote ni wakati wake na vituko mbalimbali vitaonekana kwenye mchezo wa leo.

Nipashe inachukua fulsa hii kuwakumbusha mashabiki na wanachama wa klabu hizi kushangilia timu zao kwa amani bila kuwapo kwa vitendo vyovyote vitakavyochochea uvunjifu wa amani na uhalibifu wa mali za uwanja huo uliojengwa kwa pesa nyingi.

Tunaamini Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kwa ajili ya kuimarisha hali ya ulinzi na usalama uwanjani kwa muda muda wote wa mchezo.

Lakini ni vizuri pia kuwakumbusha mashabiki wa klabu hizi kuachana na vitendo visivyokuwa na tija wakati wa mchezo huu kama kuvunja viti na vifaa vingine vya uwanja pale wanapoona timu yao haifanyi vizuri.

Ingawa kwa msimu huu bado vitendo hivyo havijaonekana, lakini ni vizuri mashabiki na wapenzi wa soka kuchukua tahadhari na kuhakikisha wanashangilia kwa amani na kiungwana mpaka mpira utakapomalizika na kuondoka wakiacha uwanja upo katika hali nzuri.

Vitendo vya ung’oaji wa viti kama ilivyotokea kwenye baadhi ya michezo msimu uliopita si vya kiungwana na havipaswi kuonekana kwenye mchezo wa leo.

Mchezo wa soka siku zote una matokeo matatu ambayo ni ushindi, sare au kufungwa hivyo mashabiki wakubaliane na matokeo yoyote watakayopata.

Kwa timu yoyote ambayo imejiandaa vya kutosha ni wazi watakuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi , mashabiki pia waache kasumba ya kuwashambulia wachezaji wao pale wanapopata matokeo yasiyofurahisha kwa upande wao.

Nipashe tunafahamu kuwatuhumu wachezaji baada ya mpira kumalizika ni kuwavunja moyo kwani asiyekubali kushindwa siku zote si mshindani.

Tunategemea mchezo wenye ushindani mkubwa tukiamini timu inayostahili ndiyo itakayopata ushindi.

Nipashe tunazitakia kila heri Simba na Yanga katika mchezo huu wa leo ambapo timu itakayoshinda itakuwa imewapa raha mashabiki wao ambao kwa zaidi ya wiki mbili kuelekea kwenye mchezo huu wamekuwa wakitaniana na kutambiana huku kila upande ukiamini wao ndio watakaoibuka na ushindi baada ya dakika 90 za mchezo.

Habari Kubwa