Tushikamane kuiunga mkono Serengeti Boys

04Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tushikamane kuiunga mkono Serengeti Boys

SERENGETI Boys - Timu ya Taifa ya Vijana, imeonyesha mwanga mzuri unaopaswa kuendelezwa ili kufufua matumaini ya Tanzania kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

Ushindi wa nyumbani na ugenini walioupata katika mechi dhidi ya Shelisheli, hauwezi kupita bila kupongezwa.
Ikiwa mbele kwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam kuwania kufuzu kucheza Fainali za Vijana

Afrika, Seregenti Boys ilipata ushindi wa mabao 6-0 katika mechi ya ugenini.

Ushindi huo umewafanya vijana wetu kusonga mbele kwa jumla ya mabao 9-0, hivyo kukutana na Afrika Kusini katika mchezo unaofuata baadaye mwaka huu.

Kama wadau wa michezo, tumefurahishwa na matokeo hayo mazuri, tukiamini msemo '"Mwanzo humalizika vizuri pia."
Tunaamini, matunda mazuri ya vijana wetu katika mechi mbili walizocheza, yametokana na maandalizi mazuri waliyopata kwenye michauno hiyo.

Mara nyingi soka letu limeshindwa kupiga hatua kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo ya maandalizi dhaifu ya timu za taifa.

Hata kwenye klabu, soka letu pia limekuwa likikumbana na hali kama hiyo na kuziacha timu kuwa wasindikizaji.

Lakini kwa kile kilichoonyeshwa na vijana wetu, tuna hakika sasa kazi kubwa ni kuhakikisha timu inaandaliwa vizuri kwa ajili ya mashindano.

TFF - Shirikisho la Soka Tanzania, kama wasimamizi wa mchezo huo, wana dhamana ya kuhakikisha vijana wetu wanaendelea kutunzwa na kupewa kila kinachowezekana kama sehemu ya maandalizi ya michuano hiyo.

Tungependa kuona TFF ikitumia muda mwingi kuiandaa timu na siyo kuunda kamati za ushindi, ambazo hazijawahi kulikomboa soka la Tanzania.

Kama wadau wa michezo, tunaamini kuwa kama vijana wetu wataendelea kuandaliwa vizuri na kupata mechi nyingi za majaribio, wanaweza kuwa alama ya ukombozi wa soka la Tanzania katika ngazi ya kimataifa.

Tungependa kuona soka letu linapiga hatua na hazina kubwa ya kujivunia kwa sasa ni Serengeti Boys.
Uwezo walioonyesha vijana wetu, umetoa tafsiri ya uwepo wa vipaji vya soka nchini.

Kama kweli tunapenda kuiona Serengeti Boys ikiendelea kufanya vizuri ni lazima kuwekeza nguvu pamoja.

Jukumu la matunzo ya Serengeti Boys halipaswi kubebwa na TFF peke yake, bali wadau wote wapenda michezo.

Ifike mahali wadau wa michezo tujione tuna deni kubwa la kuikomboa Tanzania katika medani ya kimataifa na hili litawezekana kwa kuunganisha nguvu.

Kadhalika, hii ni fursa pia kwetu kuwakumbusha vijana wetu kubaki kwenye maadili ya kimichezo na kuepuka aina yoyote ya vitendo vya utovu wa nidhamu ndani na nje ya uwanja.

Wakumbuke kuwa, hata kama mchezaji atakuwa na kipaji cha pekee na aina yake, bila kuwa na nidhamu hawezi kufika mbali.

Hivyo basi, wakati wadau tukifurahishwa na matunda ya vijana wetu, wachezaji wenyewe wana jukumu la kulinda vipaji vyao kuzingatia programu za mazoezi .

www.guardian.cotz/circulation

Habari Kubwa