Tusikubali imani za kijinga  zitukoseshe maendeleo

08May 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tusikubali imani za kijinga  zitukoseshe maendeleo

TAARIFA kwamba zahanati moja wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, imefungwa na serikali kwa zaidi ya mwezi mmoja, kutokana na hofu ya imani za ushirikina ni za kusikitisha sana.

Habari hizo zilichapishwa katika toleo letu la jana, ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, ilitangaza kuwa umeifunga zahanati ya kijiji cha King'ombe kutokana na watendaji wa zahanati hiyo kutishiwa na matukio ya kishirikina wawapo kazini.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Jacob Mtalitinya, alisema halmashauri imeamua kuifunga zahanati hiyo mpaka hapo uongozi wa kijiji utakapokaa na wakazi wa kijiji hicho ili wakubali kuachana na vitendo hivyo.

Alisema zahanati hiyo ilifungwa zaidi ya mwezi mmoja uliopita, kutokana na watumishi wa afya waliokuwa wakifanya kazi katika zahanati hiyo kulalamikia kuwapo vitendo vya kishirikina.

Alisema serikali haiamini masuala ya ushirikina, lakini kama vitendo vizuri vipo hata vibaya vipo pia, na kuwa vitendo hivyo vimejenga hofu kwa watumishi.

Mkurugenzi huyo alisema anasubiri taarifa ya kikao hicho na wakishakaa na kuonyana kuhusiana na tabia hizo, wakati wowote zahanati itafunguliwa, lakini ni vigumu kwa sasa watumishi kuendelea na kazi kwa kuwa wameingiwa na hofu.

Imedaiwa na baadhi ya watumishi wa zahanati hiyo kuwa  walikuwa wakipigwa makofi na watu wasioonekana, kuanguka kifafa na wakati mwingine walikuwa wakikuta funza wamejaa katika vyumba vya kutolea huduma.

Kutokana na mazingira hayo, walitoa taarifa kwa uongozi wa Manispaa ambao uliamua kuifunga, hatua ambayo imeelezwa na baadhi ya wanakijiji hicho kuwa imewasababishia usumbufu, kutokana na kulazimika kutembea umbali mrefu kwenda maeneo mengine kufuata huduma za afya.

Imani potofu za kishirikina ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya jamii na kama wanajamii husika hawataamua kuachana nazo, wajue kuwa watakosa maendeleo mwa kipindi kirefu, huku wenzao katika maeneo mengine wakiendelea kwa kasi.

Matukio ya kishirikina yamekuwa yakitajwa kuwa chanzo cha baadhi ya maeneo nchini kukumbwa na watumishi kadhaa wa serikali kutokana na kuhofia maisha yao, na wakati mwingine watumishi wapya huamua kukataa kwenda katika maeneo hayo wanapopangiwa kuanza kazi au kuhamishwa.

Hali hiyo pia huchangia watumishi wa umma walioko katika maeneo hayo kukosa morali wa kazi kutokana na kuishi kwa hofu na kutojiamini kutokana na imani hizo potofu.

Kimsingi, imani za kishirikina zinapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote na jamii yetu kama tunataka maendeleo, vinginevyo, maeneo yatakayoziendeleza na kuziendekeza zikubali kubakia nyuma kimaendeleo.

 

Tunasema hivyo kutokana na athari watakazozipata zikiwamo kukimbiwa na watumishi wa sekta za afya, elimu, sheria na nyingine ambazo zinagusa maisha yao moja kwa moja.

 

Hakuna mtumishi wa umma kama mwalimu, daktari, muuguzi na hakimu ambaye atakuwa tayari kupangiwa kufanyakazi katika jamii isiyostaarabika, ambayo inawatishia maisha badala ya kuwapa ushirikiano na kuishi nao vizuri.

Kibaya zaidi ni kuwa wanaoathirika zaidi kutokana na imani hizo ni wananchi wengi, ambao wanakosa huduma za afya, elimu na nyinginezo muhimu.

Kwa kuwa kwa muda mrefu suala la elimu kwa jamii kubadilika na kuachana na imani potofu kama za kishirikina, tunaona kuwa kuna haja ya jamii, wadau na serikali kuchukua hatua nyingine kususan za kisheria dhidi ya watu wachache ambao watabainika kuhusika.

Kamwe tusikubali imani za kijinga zitukoseshe maendeleo kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.

Habari Kubwa