Tusiruhusu tena kipindupindu

06Oct 2016
Mhariri
Nipashe
Tusiruhusu tena kipindupindu

KUNA taarifa za kulipuka upya kwa ugonjwa wa kipindupindu katika Manispaa ya Dodoma.

Taarifa zilizothibitishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Charles, zinaeleza kuwa juzi wagonjwa wapatao 17 waliripotiwa kuugua kipindupindu katika Hospitali yaMirembe.

Dk. Charles alisema kwamba ugonjwa huo uliibuka tena mkoani Dodoma Septemba 28, mwaka huu baada ya mgonjwa mmoja katika hospitali hiyo kugundulika kuugua kipindupindu.

Dk. Charles alisema mgonjwa huyo aliugua kwa siku mbili, ndipo madaktari walipoamua kuchukua vipimo kujua kama ni kipindupindu ama la, na kwamba wakati wakisubiri majibu ya vipimo, wengine 16 walipatwa na ugonjwa huo Septemba 30.

Hata hivyo, alisema wamejipanga kuhakikisha kipindupindu hakitoki nje ya hospitali hiyo ya magonjwa ya akili na kuiagiza manispaa ihakikishe inatekeleza mikakati yote ya kudhibiti kipindupindu.

Pia, alisema wamedhibiti mwingiliano wa watu wanaotoka nje ya hospitali ikiwa ni pamoja na kusitisha huduma ya kupeleka chakula kwa wagonjwa.
Taarifa hizo za mlipuko wa kipindupindu ni za kutisha na zinaonyesha kwamba hatua endelevu za kuutokomeza ugonjwa huo hazijachuliwa wala kupewa kipaumbele.

Mwaka jana ugonjwa huo ulilipuka karibu katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na kuua mamia ya watu na wengine kulazwa.

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Rais John Magufuli Desemba 9, mwaka jana alifuta sherehe za maadhimisho ya miaka 54 ya uhuru wa Tanzania Bara na kuelekeza watu wote wafanye usafi katika mazingira yao zikiwa ni jitihada za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo.

Agizo la Rais Magufuli lilipokelewa kwa mwitikio mzuri huku baadhi ya mikoa na wilaya zikiamua kujiwekea utaratibu wa kufanya usafi kila mwezi na nyingine kila wiki. Tangu zilipoanza kuchukuliwa hatua hizo, mlipuko wa kipindupindu ulipungua katika maeneo mengi ya nchi.

Taarifa za mlipuko mpya wa kipindupindu mkoani Dodoma zinapaswa kuwa changamoto, kwamba bado zinahitajika hatua zaidi za kukabiliana ugonjwa huo ambao chanzo chake ni uchafu.

Bila shaka mamlaka husika zitakuwa zimepata taarifa za maambukizi mapya ya ugonjwa huo na zitajipanga na kuchukua hatua za haraka kuyadhibiti kabla hayajaleta madhara zaidi, vikiwamo vifo.

Jambo la msingi la kuzingatia ni kuhakikisha kwamba maeneo yote yanafanyiwa usafi na kuzingatia kanuni za afya. Wauzaji wa vyakula wahakikishe wanafanyabiashara katika maeneo safi, wavifunike pamoja na kutumia majisafi. Wananchi wahakikishe wanakunywa maji yaliyochemshwa, waache kula ovyo vyakula vya mitaani na wanawe mikono baada ya kutoka chooni.

Kwa upande mwingine, vituo vya afya, zahanati na hospitali zitenge kambi maalumu kwa ajili ya kuwapokea na kuwatibu wagonjwa wa kipindupindu.

Njia pekee ya kuepukana na mlipuko wa kipindupindu ni usafi wa mazingira, hivyo kila mmoja popote alipo ahakikishe kwamba mazingira yake ni safi wakati wote. Hatupaswi kujidanganya kwa kuamini kuwa ugonjwa huo utatokomezwa bila kuchukua hatua endelevu za usafi wa mazingira yetu.

Mamlaka zetu hususani halmashauri zinapaswa kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kukaidi kanuni za usafi na maagizo yote yanayohusiana na usafi. Tufike mahali sasa tusiruhusu tena ugonjwa wa kipindupindu.

Habari Kubwa