Tusiwape nafasi watu wachache kuiua ATCL

30Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tusiwape nafasi watu wachache kuiua ATCL

JUZI Rais John Magufuli alizindua ndege mpya zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Ndege hizo aina ya Bombadier Q400 zilinunuliwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 500 kutoka Canada na zitakuwa zikitoa huduma katika viwanja vya ndege vya nchini vipatavyo 12 na baadhi ya nchi za nje ikiwamo Comoro.

Tunaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa umakini uliofanikisha mpango huo kwa muda mfupi tangu iingie madarakani licha ya kukumbana na changamoto za hapa na pale.

Watanzania tunapaswa kujivunia hatua hiyo kwa sababu imeirejeshea heshima nchi kutokana na huko nyuma watu wachache kuhusika katika vitendo vya hujuma zilizosababisha shirika hilo la umma kukosa ndege na lenyewe kukaribia kufa.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa ndege hizo, Rais Magufuli alieleza madudu kadhaa yaliyosababisha ATCL ifikie hapa ilipo. Baadhi yake ni wizi wa fedha na mali za shirika, udanganyifu, ajira za upendeleo na viongozi kusafiri bila kulipa nauli.

Alitoa maagizo kadhaa kwa bodi na menejimenti ya ATCL yakiwamo ya kutoruhusu kiongozi yeyote kusafiri bure hata kama ni yeye au Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, kuhakikisha kunakuwapo umakini katika uuzaji wa tiketi pamoja na kuajiri watu wenye uwezo wa kufanyakazi na kuhimili ushindani badala ya ajira za mazoea za familia, ndugu na jamaa wa viongozi.

Sura za wajumbe wa bodi mpya ya shirika hilo zinatupa matumaini kwamba ni watu watakaotumia uzoefu wao na utaalamu katika masuala ya uchumi na masoko kulisuka upya na kuliwezesha kuhimili ushindani mkubwa na kutengeneza faida, ambayo italiwezesha kujitanua ikiwamo kununua ndege mpya zaidi.

Ubunifu ni suala muhimu na miongoni mwa mambo watakayopaswa kuyapa msukumo ni ushirikiano wa biashara. Hakuna shirika lolote la ndege duniani linaloweza kutoa huduma kwa nchi zote duniani peke yake, hivyo kinachofanyika ni kushirikiana na mashirika mengine katika kutoa huduma.

Kadhalika, ATCL itapaswa kupanua wigo wa mtandao kwa maana ya kupeleka ndege zake kutoa huduma katika maeneo mengi zaidi nchini ambayo yana mahitaji ya usafiri wa anga.

Kukosekana kwa huduma bora kwa wateja pamoja na kufanyakazi kwa mazoea kwa wafanyakazi wengi ni ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kuifikisha ATCL hapa ilipo.

Kutozingatia muda wa kuruka kwa ndege, kufuta safari ovyo, lugha mbaya kwa wateja na huduma zisizoridhisha ndani ya ndege pia vilichangia kuharibu jina la shirika.

Angalizo alilolitoa Rais Magufuli linatosha kuwapa changamoto menejimenti na bodi ya shirika kukuna vicha kubuni mikakati mipya na endelevu itakayoliwezesha kukabiliana na ushindani na kuendelea kutoa huduma bora za usafiri wa anga kwa Watanzania na nje ya nchi.

Ni mafanikio hayo yatakayoifanya serikali ikubali kutumia fedha nyingine za walipakodi kuagiza ndege nyingine mbili mpya moja yenye uwezo wa kubeba abiria 160 na nyingine abiria 240 kusafiri moja kwa moja kutoka nchini hadi nchi za China na Marekani.

Uongozi na wafanyakazi wa ATCL wasikubali mtu yeyote awakwamishe kufikia malengo haya ambayo yataipaisha nchi yetu kiuchumi. Sote tusikubali kurudi tulikotoka.

Habari Kubwa