Tusiwe ‘veterani’ wa corona tuwasikilizeni wataalamu

23Feb 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tusiwe ‘veterani’ wa corona tuwasikilizeni wataalamu

WAKATI wakuu wa serikali wanatafuta njia ya kusaidia watu wasipate taharuki kisaikolojia na kiuchumi kutokana na changamoto ya corona, ni vyema viongozi wakiwamo wakuu wa mikoa, wilaya, mitaa na wenye majukumu ya afya kuwahamasisha wananchi kujikinga na kuondoa dhana na maelezo mengi potofu ...

yasiyo na tija.

Tunasema haya kwa sababu wapo vijana na hata baadhi ya watu kwa mfano wanaoendelea kusema kuwa corona ni ugonjwa wa wazee na wenye maradhi sugu na kwamba hauwapati vijana na hili linadhihirika miongoni mwa vijana hasa wanaoendesha bodaboda na bajaji.

Licha ya kukutana na abiria wengi wakiwamo wagonjwa na wanaowahudumia wanaoumwa corona, madereva hawa hawatumii barakoa na kinachoonekana ni kukosekana uhamasishaji. Haya ni mambo ambayo hayana maana. Aidha, wapo wanaowaambia watu kuwa barakoa hazisaidii. Hivi ni vitu ambavyo vinatakiwa kukwepwa na umma kuhamasishwa kwa nguvu zaidi.

Tunategemea kuwaona viongozi wakuu wakitoka ofisini na kusimamia usafi kuanzia kwenye vituo vya mabasi, mikusanyiko masokoni, minadani, kwenye kumbi na popote panapohitajika kuwa na usimamizi na ufuatiliaji ili kulinda maisha.

Ukweli ni kwamba maradhi yapo kama Rais John Magufuli, alivyosema hivyo ni lazima kuchukua tahadhari na kuzingatia maelekezo ya wataalamu na kuendelea kujiongeza kwa kujitakasa kuepuka ugonjwa huo.

Kwa mfano, pamoja na kunawa mikono kila wakati, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kukaa umbali wa mita moja kutoka mtu hadi mtu pengine ni vyema kuacha kukaa kwenda kwenye mikusanyiko isiyo na ulazima.

Aidha, ni wakati wa wenye daladala na wanaosafirisha abiria mijini kuacha kujaza abiria jambo ambalo linaweza kusababisha kasi ya kusambaa kwa magonjwa hasa mijini. Lakini ni vyema kukumbushana kuvaa barakoa hasa kwenye magari hayo kwa sababu kukinga ni bora kuliko kuponya.

Kuwahamasisha wananchi kubadili tabia na kufahamu kuwa kuingia kwenye maisha mapya. Tunategemea sasa tuone matangazo ya kuhamasisha watu kuvaa barakoa, kubadilisha nguo walizovaa wakiwa sokoni, kanisani na kazini wanapofika nyumbani na ikiwezekana kuoga mara moja ili kujiweka kwenye hali ya usalama zaidi.

Tunarajia pia kusikia watu wakikumbushwa kuacha kujimezea dawa kama wanavyopenda maana kuna wanaokula dawa (antibiotics) kila mara kujikinga, wapo wengine wanaomeza vidonge vya kuongeza kinga ya mwili. Hili ni jambo la kuangaliwa pia. Si afya kutumia dawa kwa muda mrefu bila ulazima na maelekezo ya madaktari.

Tunaikumbusha serikali hili nalo kulikemea na kuonya kwa vile kuna uwezekano wa kujenga usugu miongoni mwa Watanzania ambao pengine hawatapata corona, lakini wakawa wamekunywa dawa nyingi bila sababu.

Tunasema hayo kwa sababu kuna maelezo mengi kuhusu tiba ya corona yanayotolewa mitaani na mengine yanatekelezwa na baadhi ya wataalamu kwenye maduka ya dawa wanaowahimiza watu kutumia dawa za aina fulani kwa maelezo kuwa zinaongeza tiba.

Tunapenda kuwakumbusha watu kutumia vyakula na tiba za asilia ambazo zimeelezwa mara kwa mara na wataalamu wa dawa nchini zikihusisha kula ndimu, tangawizi, limau, nanasi, machungwa, matunda yenye rangi ya njano, karoti, mboga za majani na pia kujifukiza.

Tukumbuke kuwa huu si wakati wa kuzungumza kana kwamba ni ‘maveterani’ wa corona bali ni muda wa kusikiliza na kufuata maelekezo ya wataalamu. Tuache kudanganyana, tujikinge kama Rais anavyosema maana hivi ni vita.

Habari Kubwa