Tutaachana lini na mafuriko haya?

19Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tutaachana lini na mafuriko haya?

MAENEO mengi ya Dar es Salaam yapo kwenye hatari ya kuzama kwenye mafuriko na kila mara serikali imekuwa ikipiga mbiu ya kuwahimiza wananchi wanaoishi mabondeni wahame.

Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 inakataza kujenga mtoni au ufukweni na kuagiza mwenye kujenga karibu na mto aweke makazi yake umbali wa mita 60 kutoka mtoni bila kujali ni mjini au kijijini.

Tunaona kuwa kukaidi sheria na maelekezo ya serikali yamekuwa sababu ya watu kutumbukia kwenye mafuriko kila mwaka na imekuwa ni jambo ambalo halitibiki.

Kama Rais John Magufuli, alivyoelekeza jana nasi tunaungana naye kusisitiza kuwa kujiokoa na mafuriko ni lazima kutii sheria za nchi na mazingira ya asili.

Anasema kuwa watu wanapotaka kujenga eneo wawasiliane na wataalamu kujua ukweli wa mazingira ya asili ikiwamo mikondo ya maji na njia zake kwani kujenga juu yake kunasababisha mafuriko.

Ni vyema kukaa mita 60 kutoka mtoni au njia ya maji na pia kuachana na mazoea ya kujenga kwenye mikondo na njia hizo kwa kuwa zimekuwa tatizo kila mwaka.

Aidha, ni kosa kuizuia mikondo na njia hizo kwa kuwa ndiyo mwanzo wa mafuriko ikizingatiwa kuwa zama hizi ni za mabadiliko ya tabianchi.

Wakazi wa Dar es Salaam wameshuhudia jinsi ambavyo maji yanavyotishia maisha na kusababisha kitisho kikubwa kwa uhai kuanzia barabarani, njia za reli, mitaani na zaidi kwa wakazi wa mabondeni.

Hili siyo suala la kupuuza tena ni wakati wa kuzingatia maelekezo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na kukumbuka kila wakati kuwa taasisi hii imekuwa ikionya kuhusu mvua nyingi na kubwa zinazotarajiwa kunyesha.

Maelezo ya TMA yachukuliwe pamoja na taarifa za wataalamu wa mazingira kuhusu athari za ongezeko la joto duniani linaloambatana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa kuwa athari zimeanza kuonekana na maafa yanakuwa makubwa kila mwaka ni wakati wa serikali kuwashughulikia waliojenga juu ya mikondo ya maji, kufunga njia za maji kwa kuweka kifusi na majengo makubwa juu yake.

Mamlaka zinazoshughulikia mipango miji hazina budi kuamka na kufanyakazi kikamilifu kwani hakuna atakayeionea nchi huruma wakati wavunja nchi ni wananchi wenyewe.

Wakazi wa Dar es Salaam wanachoka, kuna mafuriko kila mwaka kwa kuwa wakazi wake wanakaidi kuondoka mabondeni wanaishi kwenye bonde la Mto Msimbazi sehemu za Kigogo, Jangwani, Mkwajuni, Tabata na Buguruni.

Hawa ni baadhi ya waathirika wa tatizo hilo kila mwaka. Ni wazi kuwa kila mwaka athari hizo zinawakumba wananchi ambao mbali na kufariki dunia nyumba zao zinabomolewa, vifaa kama magari, mifugo ikiwamo kuku na wanyama wadogo wanakufa.

Tunaona kuwa ni wakati wa kupata suluhu ya kudumu ya tatizo hilo, pamoja na kutumia taarifa za hali ya hewa serikali inaweza kuomba msaada wa kimataifa kutoka Taasisi ya International Telecommunication Union (ITU).

ITU inaweza kufanyakazi na Mamalaka ya Mawasiliano pamoja na TMA kuweka vifaa vya kuwakumbusha wananchi na kuwapa maonyo kuhusu mafuriko.

Ujumbe wa onyo na tahadhari za mafuriko kwa wananchi limekuwa likutumiwa kwenye mataifa ya Zambia na imewezekana kuokoa maisha.

Kuna imani kwamba taarifa za onyo na tahadhari zikitolewa mapema zinaweza kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi kuondoka mapema mabondeni na kuhamia milimani au maeneo salama.

Habari Kubwa