Tutizame sheria kuokoa watoto 800,000 mitaani

20Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tutizame sheria kuokoa watoto 800,000 mitaani

UNYANYASAJI kijinsia unaohusisha kutelekeza familia, vipigo, watoto kuozwa, kupewa mimba na kugeuzwa kuwa wakazi wa mitaani ni jambo lililoibuka wiki hii kwenye mjadala ulioibua taarifa kuwa takribani watoto 800,000 wanaishi katika mazingira magumu au mitaani.

Tunashukuru kuwa kasoro za kisheria ni moja ya matatizo yanayochangia matatizo kwa watoto kwa mfano, sheria ya kutunza mtoto inazungumzia zaidi kumtunza mtoto lakini haimjali mama anayetelekezwa.

Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009, sura ya 4(2) inasema kuwa maslahi ya mtoto yatakuwa ndiyo msingi wa kuzingatiwa katika masuala yote yanayohusiana na mtoto. Aidha, yatakuwa yanashughulikiwa na taasisi za umma au taasisi za binafsi za Ustawi wa Jamii, mahakama au mamlaka za kiutawala. Sheria hii haijamgusa mama ambaye ni mzazi wa mtoto.

Sura ya 26:1(a),(b),(c) inaongelea haki ya mtoto wazazi wanapotengana, upungufu unaoonekana hapa ni kwamba , mama anayetelekezwa, pamoja na mtoto wake hawajahusishwa moja kwa moja kisheria.

Inakuwa kama sheria haimfahamu mama mzazi, ndiyo maana inahitaji kufanyiwa marekebisho ili mama na familia inapotelekezwa kuwe na sheria za kumuwajibisha na kumwadhibu baba anayehusika na uvunjaji wa sheria ya kukataa familia yake inayomtelekeza mototo ambaye huishia mitaani.

Huenda kwa kutumia mwanya au udhaifu huo wanaume hupuuza kuwatunza watoto na hata kama wataitwa kwenye mashauri ya ustawi wa jamii hawaitikii wito na hawajali kutelekeza wanawake na watoto wao.

Kutelekeza watoto takribani 1,000,000 na kuwaacha waishi mitaani ni jambo ambalo serikali inatakiwa kulitafutia ufumbuzi haraka. Kama suala ni sheria zirekebishwe ili kuzuia idadi hiyo isiongezeke.

Pamoja na vipengele vya sheria ya ndoa vinavyohusu umri wa kuolewa kufutwa na mahakama ya rufani, kuna haja pia ya sheria hiyo inapoandaa vipengele vipya vya kuiboresha itoe utaratibu wa ndoa za kimila ambazo nazo zina masuala yanayotatiza hatma ya watoto.

Mara nyingi ndoa za kimila ni kama zinafanyika kwa utaratibu holela hivyo kuna haja ya kuuchunguza na kuuboresha kwa ajili ya ustawi wa watoto na mama zao.

Tunaiomba serikali kuzitazama ndoa za kimila ambazo mara nyingi zinasababisha familia kushindwa kutunza watoto ambao wengine huishia mitaani.

Hata hivyo, zama hizi kuna utaalamu na teknolojia ya kupima vinasaba polisi wanaweza kuutumiwa kutambua familia na wazazi wa watoto hao wanaoishi mitaani.

Tunaamini huu ndiyo wakati wa kufikiria namna ya kutumia kipimo cha DNA na kupata utambuzi wa watoto ili kuwawajibisha wazazi au walezi wa jeshi kubwa la watoto karibu 1,000,000 wanaoishi mitaani.

Tunashangaa na kusikitika kusikia kuwa serikali inatumia mabilioni kila mwezi kusomesha wanafunzi elimu ya msingi hadi sekondari wakati watoto wengine karibu milioni moja wanakosa huduma hiyo na wanaishi katika mazingira magumu.

Tunaona kuwa kuna haja ya kuitazama pia sheria ya mahusiano kazini ya 2004 ili kuondoa eneo la kuwanyanyasa watoto hasa mabinti na kusababisha kupata mimba wakiwa watumishi wa ndani ambao pia watoto wao huishia kuishi mitaani.

Sheria ya kazi ya 2004 inaruhusu watoto wenye miaka 14 kupata ajira na kufanyakazi nyepesi, lakini binti wa miaka 14 au 15 anapokuwa mtumishi wa ndani hunyanyaswa kupindukia.

Ajira haramu kama hizi zinatakiwa pia kumulikwa na sheria kwa vile huchangia kuongeza watoto wa mitaani ambao idadi yao sasa inaelekea kufikia milioni.

Tunaona kuwa sheria hizi zikitazamwa upya zinaweza kupunguza unyanyasaji watoto na kusababisha madhila kama kuishi kwenye mazingira magumu.

Habari Kubwa