Tutumie juhudi zote kulinda watoto

18Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tutumie juhudi zote kulinda watoto

TAKWIMU za karibuni kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),  zinaonyesha kuwa ubakaji na unyanyasaji watoto nchini unatisha.

Zinataja kuwa watoto wanaobakwa kwa siku ni 394, idadi ambayo ni sawa na watoto 2,365. Ni takwimu za kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya mwaka 2018.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zinaonyesha katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2017, matukio ya uhalifu dhidi ya watoto yalikuwa 13,457.

Hali hiyo inatisha na kama taifa si mwelekeo unaoifikisha nchi kwenye maendeleo endelevu.

Ni kwa vile watoto ambao ni tegemeo la nchi wanaathiriwa na kuumizwa kiafya na kisaikolojia.

Ubakaji na ulawiti  una matokea hasi kwa watoto kwa  mfano mimba za udogoni, kuambukizwa maradhi kama VVU na Ukimwi, kaswende na  homa ya ini.

Aidha, husababisha kisonono, kuharibu mfumo na viungo vya uzazi vya watoto na kusababisha ugumba.

Matokeo haya yanaathiri maendeleo yao kiafya, kielimu na kwenye uzazi watoto walioathirika na maradhi wanapokuwa wazazi kuna uwezekano wa kupata watoto wenye magonjwa yakiwamo VVU, upofu na homa ya ini.

 

Hili ni jambo lisilokubalika ndiyo maana tunasema ni wakati wa kila mmoja kuwalinda watoto kuanzia wazazi, walezi, jamii na taifa zima.

Tunawashauri wazazi na walezi  kuwatunza na kuwalinda watoto kikamilifu. Wawafunze jinsi ya kuepuka kunajisiwa, kubakwa na kuhakikisha kuwa watu wasiofahamika hata jamaa na ndugu zao wa karibu hawapewi nafasi ya kuwa karibu na kuwazoea watoto.

Utafiti unaonyesha kuwa ndugu na jamaa wa karibu wanahusika kuwanyanyasa watoto.

Ni wakati wa kudhibiti tabia hizo na kuachana na mienendo ya kuwaruhusu wageni hata kama ni ndugu zetu  tusio na taarifa zao kujumuika na watoto wetu hasa kwa kuwaruhusu kulala nao.

Ingekuwa vyema kuzungumza nao kuhusu ulinzi wa watoto wetu na sisi kama walezi na wazazi kusimama maisha ya watoto wetu.

Wapo watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wakitunzwa na bibi au babu, hawa ni jukumu la kijiji na wana idara ya ustawi wa jamii  kuwalinda na kuwasimamia maisha yao.

Ikumbukwe kuwa kuna wanaume wanaoa wanawake wenye watoto ili kuwanyanyasa watoto kingono.

Hili nalo ni wakati wa kulimulika na kuwachukulia hatua ili kukabiliana na tatizo hilo.

Ndiyo maana tunasitiza kuwa kupinga unyanyasaji, ubakaji na ulawiti wa watoto ni jukumu la jamii nzima na wakati umefika sasa kila mmoja kwenye nafasi yake awalinde watoto.

Kwa kuwajibika kuripoti vitendo vya unyanyasaji vilivyofichika kwenye jamii yetu.

Hatua hii ni muhimu hasa wakati huu wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo hufanyika kila Juni 16 na kaulimbiu ya mwaka huu ni hii: "Mtoto ni msingi wa taifa endelevu, tumtunze, tumlinde na kumwendeleza."

Taarifa za kitafiti kutoka LHRC zinasema kuwa Zanzibar  vitendo hivyo vinadaiwa kuongezeka.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Mkurugenzi wa Miradi ya Asasi ya Kulinda Watoto ya SOS Zanzibar, Asha Salim Ali, anasema hayo.

Anasema licha ya serikali kuwa na sheria mbalimbali, sera na mipango ya kuwalinda watoto dhidi ya aina zote za udhalilishaji, bado vitendo hivyo vinaendelea kutokea ikiwamo kubakwa na kulawitiwa.

Ni wakati wa kuchukua hatua ya kuwalinda watoto kama kaulimbiu inavyosisitiza kuwa bila watoto hakuna maendeleo endelevu.

Habari Kubwa