Tuwalinde watoto dhidi ya ajira mbaya

22Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tuwalinde watoto dhidi ya ajira mbaya

IMEBAINIKA kuwa vitendo vya ajira mbaya nchini bado ni tatizo kubwa dhidi ya watoto nchini, kutokana na kutumikishwa katika shughuli hatarishi.

Utafiti umebainisha kuwa mtoto mmoja kati ya watatu nchini, anatumikishwa katika kazi hatarishi za kiuchumi kama viwandani, kwenye mashamba makubwa, migodini na kazi za nyumbani.

Utafiti huo unabainisha zaidi kuwa asilimia 28.8 ya watoto wanatumikishwa kitaifa katika kazi za uyaya, kilimo, uvuvi na misitu, huku maeneo ya vijijini utumikishwaji ukiwa asilimia 35.6 , mijini asilimia 18 na Dar es Salaam ni asilimia 3.6.

Matokeo ya utafiti huo wa mwaka 2014/15, uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), ambao matokeo yake yalitangazwa juzi, ulibaini vilevile kuwa kuna watoto milioni 15 wenye umri wa miaka mitano hadi 17, wavulani wakiwa milioni 7.6 na wasichana milioni 7.1.

Mratibu wa Utafiti kutoka NBS, Ruth Minja, alisema watoto milioni 10.2 wako shuleni, milioni 4.4 hawako shule na milioni 2.5 hawakuwahi kwenda shule.

Alifafanua kuwa watoto milioni 4.2 ya wale ambao hawapo shuleni wako kwenye shughuli hatarishi na utumikishwaji wa zaidi ya saa 29 kwa wiki kinyume cha sheria ya mtoto na mikataba ya kimataifa.

Watoto walioko kwenye shughuli za kiuchumi ni asilimia 34.5, kati yao asilimia 94.3 ni wavulana na wasichana ni asilimia 89.6, huku kazi za nyumbani wasichana wakiwa asilimia 84.2 ambao wako kwenye uyaya na wanaume katika sekta hiyo ni asilimia 5.8.

Takwimu hizi zinatisha na zinaonyesha picha halisi kwamba kuna matatizo makubwa katika jamii yetu yanayosababisha watoto wengi kuingizwa katika ajira mbaya badala ya kwenda shule kutafuta elimu.

Kwa kuwa utafiti huo ulifanywa na taasisi za kuaminika, matokeo yake hayana shaka yoyote, hivyo Serikali itayapa umuhimu mkubwa kwa kujipanga upya kukabiliana na changamoto hizo.

Kila mtoto ana haki ya kupata elimu ili apate maarifa na ujuzi na baadaye ajitegemee kimaisha. Ndiyo maana kuna mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohimiza na kulinda haki za watoto.

Kwa mfano, ILO inazuia aina zote za utumikishaji wa watoto, ikiwamo kupiga vita ajira mbaya kupitia utekelezaji wa miradi katika nchi mbalimbali, ambayo inahamasisha na kutoa elimu kwa jamii kufahamu athari zake na kuzipinga.

Unicef pamoja na mambo mengine, imekuwa ikiweka msisitizo kuhusiana na umuhimu wa kila mtoto kupata elimu, na imekuwa ikitekeleza miradi mingi na kampeni kuhusu haki ya mtoto kupata elimu.

Jambo moja la kutilia maanani ni kwamba moja ya mambo yanayosababisha watoto kufanya kazi hatarishi ni suala la umaskini katika familia.

Wazazi wao wanaona njia pekee ni kuwatuma watoto wao kwenda kuleta kipato badala ya kwenda kusoma. Hali hiyo inakwamisha jitihada za kuwapeleka watoto shule.

Tunashauri kwamba wazazi waendelee kuhamasishwa kuhusiana na umuhimu wa kuwapeleka watoto wao shule kwa kuwa Serikali imeanza kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, na jukumu hili lisiachiwe serikali bali asasi nazo zishiriki.

Pia, sheria ziendelee kutumika kuwabana wazazi ambao wanakaidi kuwapeleka watoto wao shule, ikiwamo kuwashtaki mahakamani.

Ni matarajio yetu kuwa wahusika wamesikia na jamii nzima itachukua hatua kwa lengo la kuwanusuru watoto wetu wapate elimu badala ya kukimbilia ajira mbaya ambazo zina athari kubwa kwao.

Habari Kubwa