Tuwekeze utaalamu kwa timu za vijana

14May 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tuwekeze utaalamu kwa timu za vijana

​​​​​​​KWA hali ya kawaida kila klabu inapopambana kuhakikisha inaingiza timu yake kwenye Ligi Kuu inakuwa na malengo.

Zipo timu ambazo malengo yake ni kuwepo tu kwenye Ligi Kuu, hazina mpango wa ubingwa wala kucheza mashindano ya kimataifa. Hili ndilo kundi lenye timu nyingi, kwani humo humo ndimo hupatikana timu za kurudi Ligi ya Championships na hadi Daraja la Kwanza.

Malengo ya aina hii yana maeneo mawili. Moja ni nyenzo kwa maana ya rasilimali uchumi, kwani ili ucheze michuano ya kimataifa unahitaji mamilioni ya fedha.

Mfano ni gharama kubwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini vilevile ni faida kwa timu itakayofanikiwa kuwa bingwa kwani inapata fedha nyingi kuliko zile ilizotumia.

Hivyo kuna sababu za msingi kuingia katika mashindano ukiwa na malengo. Klabu inaweza kutumia nguvu nyingi kuhakikisha inacheza mashindano ya Afrika, lakini ikashindwa kusafiri kwenda kwenye mechi kutokana na kutokuwa na nguvu za kiuchumi.

Kwa Tanzania Bara tunao mfano wa timu za aina hiyo ambazo CAF hulazimika kuzipiga faini nzito.

Lakini bado timu inayo fursa ya kupigania ubingwa na kuupata, lakini baadaye ikasema haina uwezo kiuchumi kucheza mashindano ya CAF na nafasi yake kupewa timu inayoifuatia baada ya msimamo wa mwisho wa ligi.

Eneo la pili ni la ufundi. Kwa mpira wa miguu, si klabu tu bali hata timu za taifa unapotafuta kocha ni lazima ujue malengo ni nini vinginevyo ni wazi hakitatokea kile ambacho uongozi unakitarajia kuhusiana na matokeo ya uwanjani.

 

 

Katika timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, kuna timu zenye makocha wa kigeni.Nini mchango wa makocha hao? Kwa haraka haraka waajiriwa hao (makocha) na waajiri wao wana sababu moja tu ya kuelezea mafanikio yao.

Pia wachezaji wa timu ya Taifa ya wakubwa (Taifa Stars) asilimia kubwa wanatoka katika klabu za ndani. Kwa lugha nyepesi ubora wa wachezaji katika klabu, hasa za Ligi Kuu ndiyo ubora wa timu za Taifa, hasa Taifa Stars.

Kwa vile mpira wa miguu ni biashara kubwa na nzuri, bado kuna kila sababu kwa klabu zetu kuwekeza zaidi kwa timu za vijana. Huku faida ni kubwa zaidi kuliko hasara.

Kuwekeza kwa vijana kunatoa fursa kwa wachezaji kupata msingi mzuri wa mpira wa miguu wakiwa bado wadogo.

Lakini vilevile kuwekeza huko kwenye vitalu ni biashara nzuri ingawa inahitaji kusubiri na uvumilivu wa kutosha ili kutoa mchezaji au wachezaji wanaoweza kupeleka faida katika klabu husika na pia timu ya Taifa.

Kuajiri makocha kwa ajili ya ubingwa tu hakuna faida kama kuwaajiri kwa ajili ya programu za vijana. Programu za vijana ni uwekezaji, na matunda yake yanachukua muda mrefu kuonekana, lakini pia yakishaonekana yatadumu kwa muda mrefu.

Mpira wa miguu kama ilivyo michezo mingine nguzo yake kuu ni kuwa na wachezaji ambao uwezo wao wa kucheza na kasi viwe ni vitu vinavyoongezeka badala ya kupungua. Kwa mantiki hiyo wanahitajika zaidi wachezaji vijana, kwani hao ndiyo miili yao inaruhusu wawe na kasi uwanjani.

Wachezaji wenye umri mkubwa au wakongwe wanahitajika kwenye timu kwa ajili ya ujuzi na uzoefu wao, lakini si kwa ajili ya kasi. Mpira wa miguu wa kisasa unahitaji kasi uwanjani, hivyo hilo haliwezi kuepukika kwa kocha yeyote.

Wastani wa umri wa wachezaji vijana katika timu unatakiwa kuwa angalau asilimia 70 dhidi ya 30 za wachezaji wakongwe na wazoefu. Nafasi za wakongwe nazo hujazwa na vijana baada ya muda mfupi.

Kwa mafanikio ya muda mfupi makocha wa mataji wanayo fursa katika mpira wa miguu Tanzania. Lakini kwa tulipo hivi sasa kwa hakika tunahitaji zaidi makocha wa maendeleo ya mpira wa miguu kuliko wale wa kuleta mataji.

Habari Kubwa