Twiga Stars peperusha vyema bendera ugenini

23Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Twiga Stars peperusha vyema bendera ugenini

KALENDA ya mashindano ya kimataifa kwa upande wa ngazi ya nchi inaendelea leo ambapo Timu ya Soka ya Taifa ya Wanawake maarufu Twiga Stars inatarajia kushuka ugenini Afrika Kusini kurudiana na wapinzani wao, Namibia.

Timu hizo zinakutana katika kusaka nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake ambazo zitachezwa mwakani.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, wageni waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Kwa matokeo hayo, Twiga Stars ambayo inafundishwa na Kocha Mkuu, Bakari Shime na hivi karibuni ilitwaa ubingwa wa mashindano ya COSAFA, bila kupoteza mchezo hata mmoja, inahitaji kupata ushindi mnono ili kusonga mbele katika michuano hiyo.

Hata hivyo leo timu hizo mbili zinakutana katika uwanja huru, baada ya Namibia kuuchagua Uwanja wa Soweto ulioko Afrika Kusini kutumika kama uwanja wake wa nyumbani.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani kwa pande zote mbili, lakini Twiga Stars inaonekana itakuwa kwenye presha zaidi kwa sababu itahitaji kufuta makosa waliyofanya katika mechi yao ya awali ambayo walicheza mbele ya mashabiki wao.

Katika mpira wa miguu lolote linaweza kutokea na kinachoweza kutoa majibu sahihi ni kusikia filimbi ya mwisho baada ya kumalizika kwa dakika 90.

Tunaamini Shime na benchi lake la ufundi limeshayafanyia kazi upungufu yote na leo watashuka uwanjani wakiwa makini na wenye utulivu wa kuhitaji 'kupindua meza' na hatimaye kuendelea katika hatua inayofuata ya mashindano hayo yanayosimamiwa na kuandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kama Namibia walicheza vyema na kupata ushindi wakiwa kwenye ardhi ya Tanzania, basi hilo linawezekana kwa Twiga Stars kupambana na hatimaye kuwaondoa wapinzani wenu kwenye michuano hiyo mikubwa inayoendelea hapa barani Afrika.

Soka ni suala la kujipanga vyema na kutumia vizuri nafasi ambazo mtazitengeneza, utulivu na umakini ndio silaha kuu ambayo inaweza kuwafanya Twiga Stars mkamaliza dakika 90 zilizobakia za ugenini mkiwa na shangwe ambayo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki na wadau wa soka hapa Tanzania.

Mbali na Twiga Stars, Simba, Azam FC na Biashara United pia zinakabiliwa na majukumu ya kimataifa katika mechi za marudiano za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Klabu hizo zilipata matokeo mazuri katika mechi zao za kwanza, lakini tunawakumbusha kuwa bado hawajamaliza kazi mpaka watakaposikia filimbi ya mwisho imelia.

Kuna wakati mpira unakupa matokeo katili, ili matokeo hayo yasije kwa upande wa klabu za Tanzania, ni vyema wachezaji wakajipanga kujituma kusaka matokeo chanya na kumalizia kazi nzuri ambazo walizianza.

Kufanya vyema kwa timu hizo, zitaihakikishia Tanzania kupata uwakilishi wa klabu nne katika mashindano hayo ya kimataifa mwakani na kama zote zitashindwa kuingia makundi, basi tutajiweka kwenye nafasi ya sintofahamu.

Tayari Azam ilishafika Misri kwa ajili ya kurudiana na Pyramids wakati Simba itakayowakaribisha Jwaneng Galaxy kutoka Botswana yenyewe imeshakaa sawa na imara kuendelea pale ilipoishia, lakini Nipashe ikiwataka Biashara United kuongeza umakini watakapokuwa ugenini kurejeana na Al Ahly Tripoli.

Tunawakumbusha mpira ni ajira, hivyo wachezaji wa timu zote zinazokabiliwa na mashindano ya kimataifa wanatakiwa kucheza kwa viwango vya juu ili kujiweka sokoni au kumvutia Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen kuwaita kwenye kikosi chake.

Habari Kubwa