Uamuzi wa kuifuta CDA umefanywa wakati mwafaka

17May 2017
Mhariri
Nipashe
Uamuzi wa kuifuta CDA umefanywa wakati mwafaka

RAIS John Magufuli, ameivunja rasmi Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na kuagiza mali na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na mamlaka hiyo zihamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.

Rais ameivunja CDA kwa kutia saini hati ya Amri ya Rais ya kuivunja Mamlaka hiyo, akisema ameamua kuivunja na kuhamishia majukumu yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji wa huduma kwa wananchi uliokuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili na pia kuendana na mahitaji ya sasa ambayo yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya kuwapo kwa CDA.

Aidha, Rais Magufuli alitangaza kuivunja Bodi ya CDA, na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Paskasi Muragili, atapangiwa kazi nyingine na ameagiza wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo wahamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na ofisi nyingine za Serikali kadri inavyofaa.

Pia, Rais aliagiza hati zote za kumiliki ardhi zilizokuwa zikitolewa na CDA kwa ukomo wa umiliki wa miaka 33 zibadilishwe na kufikia ukomo wa umiliki wa miaka 99 kama ilivyo katika maeneo mengine nchini ili kuwavutia wawekezaji hasa wa viwanda.

Ni ukweli kwamba kuwapo kwa mamlaka mbili yaani CDA na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kulikuwa kunasababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi na kushindwa kuelewa ni mamlaka ipi walipaswa kwenda kupata huduma mbalimbali zikiwamo za ardhi.

Hali hiyo ilikuwa ikisababisha malalamiko ya wananchi dhidi ya CDA na kuna wakati baadhi yao walidiriki kutoa kauli kwamba mamlaka hiyo ndiye adui yao namba moja.

Rais Magufuli juzi wakati akitangaza uamuzi huo mbele ya viongozi waandamizi wa serikali akiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mawaziri, alisema wazi kuwa wakati wa kampeni mwaka 2015, alipokea malalamiko ya wakazi wa Dodoma kuhusiana na suala hilo na kwamba aliwaahidi kulishughulikia.

Sababu nyingine ya kupongeza hatua ya uamuzi huo ni ukweli kuwa ni chombo kilichoanzishwa kwa amri ya Rais, hivyo kushindwa kuwajibika kwa mamlaka yoyote ya mkoa wa Dodoma wakiwamo madiwani ambao wanachaguliwa na wananchi.

Pia sheria ya CDA ya kumilikisha ardhi kwa miaka 33 haikuwa rafiki kwa wawekezaji kutokana na kuwa kipindi kifupi, tofauti na mamlaka nyingine kama halmashauri ambazo muda wa umilikishaji ni miaka 99. Bila kuchukuliwa uamuzi huo, jitihada za serikali za kuwashawishi na kuwahamasisha wawekezaji hususani wa kujenga viwanda kuja na kuwekeza nchini zingekuwa bure.

Tunasisitiza kwamba Rais Magufuli ameona mbele kwa kufanya uamuzi huo kwa maslahi ya wengi kwa kutumia mamlaka yake aliyopewa kisheria, hivyo kuondoa mkanganyiko wa kuwapo mamlaka mbili ya CDA iliyoanzishwa mwaka 1973 na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230 pamoja na Manispaa ya Dodoma iliyoanzishwa kisheria mwaka 1980.

Tunaamini sasa wakazi wa Manispaa ya Dodoma watapata huduma nzuri kutoka Manispaa hiyo bila kuwapo na mkanganyiko wowote kama ilivyokuwa awali.

Suala la msingi ambalo serikali itapaswa kulitekeleza kwa usimamizi wa karibu sana ni mchakato wa kuhamisha majukumu ya CDA kwenda Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Ni matumaini yetu kuwa hilo litafanyika kutokana na ahadi aliyoitoa Makamu wa Rais.

Kama alivyosema Rais Magufuli, uamuzi huo hauna mshindi kati ya CDA na Manispaa ya Dodoma, bali wote wameshinda, hivyo kilichobaki ni watumishi wote kushirikiana na kufanya kazi kama timu moja ya kuwahudumia vizuri wakazi wa Manispaa Dodoma kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili kama makao makuu ya nchi na serikali.