Uchaguzi mitaa utuletee waadilifu

23Oct 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Uchaguzi mitaa utuletee waadilifu

KATIKA harakati za kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, tunaona kuwa taifa limejaa watu wengi wanaotamani kuwa viongozi wa kisiasa wanaotaka kubebeshwa jukumu la kuviongoza vijiji, mitaa na vitongoji.

Hilo ni bayana kutokana na ushindani mkubwa unaoonekana miongoni mwa wagombea.

Lakini, ni wazi kuwa si wanasiasa wote wanaofaa kuwa viongozi bora, wengi wanakosa vigezo muhimu kama uadilifu na uwajibikaji.

Kwa viongozi wengi ambao hawana vigezo hivyo, kinachojiri ni kila mmoja kuendeleza uzalendo wa kuchumia tumbo na kujinufaisha wenyewe wala si taifa.

Ndiyo maana wakati mwingine tunaungana na baadhi ya vyama tukiamini kuwa ni vyema kufuatilia mwenendo wa mchakato wa kuchuja majina na kufahamu wagombea walivyopatikana.

Na ikibidi kama kuna ujanja ujanja, uliofanyika wasio na sifa wanafutwa na zoezi kurudiwa upya, kama CCM ilivyofanywa kwa wagombea wote wa mkoa wa Dar es Salaam.

Si vyema kuhukumu lakini, kuna malalamiko mengi yanayotolewa dhidi ya wanasiasa kwa ngazi zote hata za serikali za mitaa.
Watu wengi wanawachukulia wanasiasa ambao ni viongozi muhimu kuwa ni wadanganyifu, wazushi na zaidi wasioaminika na wanaopata uongozi kupitia rushwa au kwa ujanja ujanja lengo lao likiwa kujinufaisha hasa kwa kusaka mali.

Tunapenda kuwaambia wapiga kura kuwa wanasiasa wote wakiwamo viongozi wa serikali za mitaa ni muhimu.

Tena wapo waadilifu na wawajibikaji, hivyo ni jambo jema kupiga kura ili kuwachagua kama ilivyo kwenye kura za maoni za kuwapitisha.

Kwa hiyo ni vyema kwa vyama vya siasa kuwa na mchakato makini wa kuwapata wagombea hao.

Zoezi hilo ni muhimu likafanyika kihalali na kwa taratibu na si kiubabaishaji hadi kusababisha matokeo kufutwa.

Ni vizuri kupata viongozi ambao si wala rushwa au ‘wapigaji madili’, kuwa na viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa wanaoingia madarakani kupitia njia za kiujanja ujanja, ambao si watumishi wa wananchi bali wanaojinufaisha, haikubaliki.

Tunasema haya kwa sababu wapo watu wanaopata uongozi kwa kutoa rushwa ya ngono kwa kamati za kuchuja majina ili wapitishwe.

Lakini, pia wapo wanaotoa rushwa ya pesa ili majina yao yapitishwe na kuna wanaowahonga wapiga kura ili wawachague, yote haya yanasababisha kupata viongozi wasio waadilifu wala wawajibikaji.

Viongozi wa kisiasa ni muhimu ambao ndiyo muhimili wa dola-kwa maana ya serikali. Tunawahitaji kama walivyo wabunge na mahakama.

Hawa ndiyo watu muhimu kwenye ngazi za mitaa, vijiji na vitongoji wanaohusika na bajeti, mipango ya maendeleo na pia ndiyo wahusika wakuu kwenye utawala na uongozi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Tunapenda kuwakumbusha wanaoogombea kuwa uongozi katika ngazi hii ni muhimu kwa kuwa ndiyo unaohusika moja kwa moja na wananchi.

Viongozi hawa wanatakiwa kuwatumia wananchi na kulitendea taifa mambo mema kama kuleta umoja na mshikamano, kudumisha upendo, uelewano, uzalendo na utaifa pamoja na kuhimiza maendeleo ili kuondokana na umaskini.

Tunapenda kuwakumbusha wanaogombea uongozi kuwa viongozi bora ni wale mchanganyiko wa karama (charisma) na uadilifu na pia uwezo wa kuchanganua mambo na kufanya maamuzi yenye manufaa ya wengi na si ya mtu mmoja.

Tunapenda kuwakumbusha kuwa uwajibikaji ni muhimu na hilo ndilo liwe msukumo kwa viongozi wa serikali za mitaa. Wakubali kukosolewa na kurekebishwa na hata ikibidi wajiuzulu madaraka yao kutokana na makosa yaliyofanyika.

Tunawatakia kila la kheri wagombea serikali za mitaa watakaoleta uongozi bora.

Habari Kubwa