Uchaguzi TFF umepita, sasa tushirikiane kuinua soka letu

09Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Uchaguzi TFF umepita, sasa tushirikiane kuinua soka letu

HATIMAYE juzi, Jumamosi wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wametimiza wajibu wao kisheria kuchagua viongozi wapya watakaobeba dhamana ya kusimamia na kuongoza mpira wa miguu nchini kwa kipindi kingine cha miaka minne.

Katika uchaguzi huo uliofanyika jijini Tanga, Rais aliyemaliza muda wake, Wallace Karia, alifanikiwa kutetea kiti chake huku kwa mujibu wa Katiba ya TFF, Karia alitangaza wajumbe wanne wa kuteuliwa ambao ni Athumani Nyamlani, Ahmed Mgoyi, Saidi Soud na Hawa Mniga, aliyekuwa mgombea pekee mwanamke katika nafasi ya urais kwenye uchaguzi huo, lakini akaondolewa hatua za awali kwa kutokidhi vigezo.

Aidha, kwa mujibu wa katiba pia Karia alimteua Nyamlani kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa shirikisho hilo, na wajumbe wa mkutano mkuu walimthibitisha pasi na shaka kuendelea kukalia kiti hicho.

Wajumbe wengine waliokuwa wakigombea nafasi sita za Kamati ya Utendaji na kuibuka washindi ni Lameck Nyambaya, Khalid Abdallah, James Mhagama, Mohammed Aden, Vedastus Lufano na Issa Bukuku.

Kwa ujumla hilo ndilo jopo la uongozi mpya litakalobeba dhamana ya kufanya maamuzi ya mwisho katika soka letu, hivyo ni wakati sasa wakuweka tofauti zetu kando za kidini, kisiasa, kiitikadi, lakini kuvuja makundi yote ya kampeni ili kuwa kitu kimoja.

Nipashe tunaamini ushirikiano kwa viongozi na wadau wote wa soka pamoja na Watanzania kwa ujumla, ndiyo silaha pekee itakayoliwezesha soka la Tanzania kupiga hatua mbele zaidi na kuwa na ligi yenye ushindani mkubwa na kuifanya kupanda kutoka nafasi ya nane ambayo inashika kwa sasa katika viwango vya ubora barani Afrika.

Lakini pia tunaamini wote waliogombea nafasi mbalimbali tangu mwanzo wa mchakato wa uchaguzi huo ulipotangazwa Juni 8, mwaka huu hadi waliokosa kura za kutosha juzi, kwetu sisi wote ni washindi na mchango wao wa maoni ama mawazo ni muhimu sana katika kulisukuma mbele gurudumu la soka letu.

Hatutarajii kuona makundi ama viongozi waliopitishwa na mkutano mkuu wakikosa ushirikiano kutoka pande yoyote ile, na watakaofanya hivyo kwetu daima ni wasaliti katika maendeleo ya soka na hawana budi kupigwa vita vikali.

Tunaamini Karia, Nyamlani pamoja na wajumbe wa Kamati ya Utendaji pekee, hawawezi kutosha kuliongoza soka pasipo kupata ushirikiano wa wadau wote wa soka na Watanzania kwa ujumla ili kuweza kufikia malengo yao ya kuona Tanzania inakuwa moja ya nchi zilizopiga hatua kubwa kisoka duniani.

Licha ya kutambua hakuna binadamu aliyekamilika, lakini busara na hekima zinapaswa kuchukua hatua zaidi pindi tunapowasilisha maoni na mawazo yetu pale tunapoona viongozi hao wameteleza katika kufanya maamuzi mbalimbali.

Pamoja na hayo neno letu kwa viongozi waliochaguliwa na kuteuliwa, hawana budi kutambua cheo ni dhamana, hivyo kutenda haki na si kutenda tu bali pia tunataka kuona haki ikitendeka kwa sheria na kanuni zilizopitishwa kwa maslahi mapana kwa wote.

Kadhalika, ili kuhakikisha viongozi hao wanatekeleza wajibu wao ipasavyo, ni wakati sasa wa wanachama wote wa TFF, klabu na wadau wao wote kufuata na kutii sheria na kanuni walizojiwekea kwani kwa kufanya hivyo kutaondoa manung'uniko yasiyo ya lazima.

Nipashe tunawataki kila kheri viongozi wote waliochaguliwa na kuteuliwa katika kuanza kutekeleza majukumu yao na mafanikio makubwa kwa kuhakikisha soka la Tanzania linapiga hatua zaidi.

Habari Kubwa