Uchukuaji sheria mkononi ukomeshwe

10Jan 2017
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Uchukuaji sheria mkononi ukomeshwe

WATU wawili wanaotuhumiwa kuwa majambazi waliuawa wakati wakihojiwa katika ofisi ya Mtendaji wa kijiji cha Lupa Market, kata ya Ifumbo wilayani Chunya mwishoni mwa wiki iliyopita na miili yao kuteketezwa kwa moto na wananchi waliojichukulia sheria mkononi.

Watuhumiwa hao waliuawa baada ya kutuhumiwa kuvamia maeneo ya wachimbaji wadogo wa dhahabu kijijini hapo, mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa Mtendaji wa Kijiji cha Ifumbo, Emily Rajabu, waliouawa ni Tegemea Henry (34), mkazi wa Kijiji cha Lupa Market na Paschal Simchimba (29), mkazi wa Mjele.

Kuuawa kwa watuhumiwa hao katika mazingira hayo, imeanza kuwa jambo la kawaida katika jamii nchini.

Kimsingi, matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara licha ya makamanda wa polisi wa mikoa mbalimbali kukemea tabia hiyo mara kwa mara katika mikutano yao na waandishi wa habari.

Katika tukio la mwishoni mwa wiki, imeelezwa, watuhumiwa hao walipelekwa ofisini kwa Mtendaji baada ya kukamatwa kwenye machimbo ya dhahabu usiku wa kuamkia janga hilo, na wakati wakiendelea kuhojiwa ghafla wananchi walivamia ofisi hiyo na kuanza kuwashambulia kwa mawe na fimbo hadi kuwaua.

Baada ya mauaji hayo, wananchi hao waliiteketeza kwa moto miili ya watuhumiwa hao, baada ya kuivalisha matairi ya gari, kuilundikia, kuimwagia petroli na kisha kuilipua kwa kibiriti.

Ni kwa nini matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara licha ya makamanda wa polisi wa mikoa mbalimbali kukemea tabia hiyo mara kwa mara?

Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara, Nipashe tunaona, kwa sababu hapajawa na mpango mkakati wa kukomesha tabia hiyo iliyozoeleka sasa nchini.

Ni vyema kwamba makamanda wa polisi wa mikoa mbalimbali wamekuwa wakikemea tabia hiyo mara kwa mara katika mikutano yao na waandishi wa habari.

Lakini kukemea peke yake, Nipashe tunasema, hakutoshi.

Ili matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi yapungue angalau, achilia mbali kukoma, Nipashe tunaona, lazima watuhumiwa wa mauaji ya watuhumiwa wajazwe hofu ya mkondo wa sheria.

Ili matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi yapungue angalau, lazima watuhumiwa wa mauaji ya watuhumiwa wajue kuwa Jeshi la Polisi litaweka kipaumbele katika kuwafikisha mbele ya sheria wao kama mtuhumiwa mwingine yeyote wa makosa ya mauaji.

Na ili kufika mahali ambapo watuhumiwa wa mauaji ya watuhumiwa watajua Jeshi la Polisi 'litalala nao mbele' kama mtuhumiwa mwingine yeyote wa makosa ya mauaji, jambo moja ni muhimu:

Jeshi la Polisi kuongeza mifano ya hatua ambazo zimewakumba wananchi waliojichukulia sheria mkononi na kuua wengine, baada ya kukamilisha haraka upelelezi wa matukio hayo.

Habari Kubwa