Uhakiki wa vituo vya yatima uamuzi sahihi

27Jun 2017
Mhariri
Dar es salaam
Nipashe
Uhakiki wa vituo vya yatima uamuzi sahihi

KATIKA jitihada zake za kuhakikisha kwamba kuna uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha zinazotolewa kwa baadhi ya asasi, serikali imeamuru kufanyika kwa ukaguzi wa fedha na kufuatilia vituo vya watoto yatima.

Uhakiki huo utavihusu vituo vyote vya kulea watoto yatima nchini lengo likiwa ni kujiridhisha kama kuna uwajibikaji na uwazi  wa matumizi ya fedha zinazotolewa na taasisi na watu binafsi kusaidia vituo hivyo.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya, alipokuwa akizindua kituo cha kulelea watoto yatima cha Dunia yenye heri kilichopo Kimbiji, Wilaya ya Kigamboni jijini  Dar es Salaam.

Alisema ni vema kufanya ukaguzi huo ili kujiridhisha namna fedha hizo zinavyotumika ili kuhakikisha kusudi la kuanzishwa kwa vituo hivyo linazingatiwa.

Alisema kuwa serikali inathamini sana mchango wa vituo vya watoto yatima ambavyo vimekuwa vikisaidia watoto ambao wanakumbwa na shida ya kupoteza wazazi wao, lakini inahitaji kuona vinafanya kazi kwa ufanisi na kama kuna baadhi ya vituo vinavyofanya kazi kwa manufaa ya mtu binafsi ivitambue.

Vituo vya kulea watoto yatima vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini vinatoa mchango mkubwa ambao hauna mfano, kutokana na kuwahifadhi na kuwapa mahitaji muhimu ya kibinadamu kama chakula, mavazi, malazi sambamba na huduma za afya na elimu.

Vile vile vituo hivyo ndivyo vinavyotoa huduma muhimu ya malezi kwa watoto hao ambao wamekosa fursa ya kupata malezi na maadili mema kutoka kwa wazazi wao.

Itakumbukwa kuwa kazi ya kulea mtoto ilivyo ngumu hadi afikie umri wa kujitegemea. Ni kazi inayohitaji moyo na uvumilivu wa hali ya juu.

Ndiyo maana watoto wengi wanaopoteza baba na mama wanapelekwa kulelewa kwenye vutuo hivyo kutokana na ndugu kushindwa kutekeleza jukumu hilo.

Tunatoa pongezi kwa vituo hivyo ambavyo vimewalea watoto wengi na kuwapa maadili mema na kujitambua, hivyo kuanza maisha ya kujitegemea na kupata mafanikio.

Hata hivyo, yamekuwapo malalamiko kadhaa dhidi ya vituo vingi vya kulea yatima. Malalamiko hayo yanahusu kutokuwapo kwa uwazi kuhusiana na misaada unayotolewa pamoja na matumizi yake.

Kukosekana kwa uwazi kuhusu misaada inayopelekwa katika vituo hivyo pamoja na matumizi yake matokeo yake ni wahusika kushindwa kuwajibika katika kuisimamia.

Baadhi ya wanaoendesha vituo hivyo wamekuwa wakilalamikiwa kuwa wanavitumia kwa manufaa yao binafsi lengo likiwa kupata na kujinufaisha na misaada zikiwamo fedha kutoka serikalini, taasisi za ndani na za nje pamoja na wasamaria wema.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wasamaria wema wanavunjika moyo wa kuendelea kutoa misaada ya kuwasaidia watoto hao na matokeo yake kukabiliwa na hali ngumu.

Ni ukweli usiopingika kuwa vituo vya yatima vinapokea misaada mingi, lakini uendeshaji wake hauendani na uhalisia, hivyo kuibua hisia kwamba misaada hiyo inachakachuliwa na kupotea maana halisi ya kusaidiwa.

Hali hiyo ndiyo iliyoifanya serikali ione umuhimu wa kufanya uhakiki wa vituo vyote vya kulea yatima kuhusu masuala ya kifedha na kama vinaendeshwa kwa uwezo na uwajibikaji.

Tunakubaliana na uamuzi huo kwa kuwa lengo lake ni kuhakikisha vituo hivyo vinaendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kukidhi lengo la kuanzishwa kwake.

Ni matumaini yetu utawekwa utaratibu mzuri wa kufanya uhakiki huo na ushauri wetu ni kwamba vituo vitakavyobainika kukosa uwazi na uwajibikaji vichukuliwe hatua ikiwamo kufungwa.

Habari Kubwa