Uhamasishaji muhimu kwa chanjo ya corona

10Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Uhamasishaji muhimu kwa chanjo ya corona

MWISHONI mwa mwezi uliopita, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi kampeni ya taifa ya chanjo ya Uviko-19 na kuwa wa kwanza kuchanjwa, kwa lengo la kuuhakikishia umma kuwa chanjo hiyo ni salama.

Baada ya uzinduzi huo wa chanjo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi, anasema, uzinduzi wa utoaji chanjo mikoa yote ulikamilika Agosti 4, mwaka huu.

Katika taarifa yake kuhusu maendeleo ya usambazaji na utoaji wa chanjo hiyo aliyoitoa juzi, anasema, tathmini inaonyesha kuwapo kwa mwitikio mkubwa wa wananchi kupata chanjo hiyo.

Kwa mujibu wa katibu huyo, rekodi ya makundi ya walengwa peke yake, kufikia Agosti 7, mwaka 2021 ilionyesha zaidi ya 164,500 walikuwa wameshajiandikisha kwa ajili ya kupatiwa chanjo wiki hii, huku wengine 105,745 wakiwa tayari wameshapatiwa chanjo kufikia tarehe hiyo.

Sisi tunaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali za kusambaza chanjo hiyo, ili kuhakikisha Watanzania wanaipata kwenye maeneo yao kulingana na maelekezo bila kikwazo chochote.

Hata hivyo, tunadhani kuna haja ya kuongeza jitahada zaidi, ili kusaidia kuongeza idadi ya watu kujitokeza kuchanjwa, kuliko ilivyo sasa, kwani haiendani ya wingi wa Watanzania ambao ni zaidi ya milioni 60.

Tunashauri kuwapo kwa uhamasishaji kila kona ya Tanzania ili watu waone umuhimu wa kwenda kuchanjwa, kwani tunadhani kwamba ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu chanjo unaweza kuchangia hali iliopo sasa.

Si vibaya elimu ikatolewa kwenye minada, vituo vya mabasi na maeneo mengine ya mikusanyiko ya watu ikiwamo hata matamasha ili kuongeza kasi ya watu kwenda katika vituo kwa ajili ya kuchanjwa.

Vilevile, tunadhani hata viongozi wa serikali za mitaa nao wana wajibu wa kutoa elimu katika maeneo yao na ikiwezekana waingie nyumba kwa nyumba ili wananchi wahamasike na kujitokeza kwa wingi.

Tunajua kuwa, kwa namna moja au nyingine, elimu ambayo baadhi ya Watanzania wameipata miaka ya nyuma kuhusu kinga ya corona, inaweza kuwafanya baadhi yao kusita kujitokeza kuchangwa.

Ni kweli suala la chanjo ni hiari, lakini inawezekana wengine wakawa hawajitokezi kuchanjwa kwa sababu tu ya elimu ambayo wamedumu nayo tangu ugonjwa huo ulipoingia nchini.

Kwa mantiki hiyo, tunaona kuna haja kuwapo kwa uhamasishaji unaokwenda sambamba na utoaji wa elimu sahihi kuhusu madhara ya ugonjwa huo na kinga yake ili Watanzania waondokane na 'giza' lililopo.

Tunaamini kwamba hayo yakifanyika idadi ya Watanzania watakaochanjwa itaongezekana na wengine wataendelea kujitokeza zaidi kujiandikisha na kuwa kwenye foleni ya kusubiri kuchanjwa.

Ni kweli huo mwanzo kwa watu waliojitokeza kuchanjwa ni mzuri, lakini tunaamini kuwa kasi zaidi inahitajika, hasa ikiendana na elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kupata chanjo hiyo.

Habari Kubwa