Uhusiano mwema uwe msingi kuinua taaluma Gairo

30Jun 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Uhusiano mwema uwe msingi kuinua taaluma Gairo

WIKI iliyopita gazeti hili liliripoti kwa kina habari ya walimu wa Shule ya Sekondari Iyongwe, Kijiji cha Chihwaga Kata ya Itaragwe, wilayani Gairo, mkoani Morogoro, kupigwa mishale na watu wasiojulikana na mmoja kupoteza maisha.

Aidha, mwalimu mmoja akiwa hospitali kuuguza majeraha baada ya kushambuliwa akitoka kwenye shughuli zake eneo lile lile aliloshambuliwa mwalimu mwenzake.

Tukio hilo linadaiwa ni la kulipiza kisasi kwa kuwa mwalimu wa pili alikubali kutoa ushahidi polisi dhidi ya mwenziye aliyeuawa, jambo linalodaiwa kuwaudhi waliotenda kosa hilo.

Mwalimu huyo alieleza lengo la wahusika lilikuwa kumuua, lakini alichomwa mkuki kwenye mkono.

Mwalimu wa kwanza aliuawa Februari 24, mwaka huu na mwingine alijeruhiwa Juni 20, wote kutoka shule moja jambo ambalo lililozua taharuki na hofu kwa walimu waliobaki.

Baada ya vyombo vya habari vya IPP kuripoti kwa kina tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, alifanya ziara na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo, ikiwamo kusalimisha silaha za jadi ambazo zinatumika kushambulia walimu hao.

Tunapongeza uamuzi wa Jeshi la Polisi kuweka kikosi maalum kinachoongozwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa, na sasa hatua za kisheria zitakuchukuliwa kwa wote waliohusika.

Tunaamini pamoja na hatua hizi za ngazi ya mkoa katika eneo hilo kuna viongozi wa wilaya ambao ni Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na viongozi wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama ambao wanaunda kamati ya ulinzi na usalama.

Pamoja na hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo kufanya uchunguzi, bado kuna uhasama baina ya walimu na wenyeji huku wote wakitegemeana. Walimu wanatakiwa kufanya kazi wapate mshahara na wazazi wanahitaji watoto wao kufundishwa.

Kama walimu watashindwa kuishi kwa amani, hawataweza kufanyakazi inavyotakiwa, watashindwa kuwafundisha kwa moyo wanafunzi ambao wanatokana na jamii hiyo.

Hali hiyo ya uhasama ikiachwa kuendelea bila kutibu majeraha yanayoonekana na yasiyoonekana katika kujenga uhusiano mwema, kuna uwezekano mkubwa wa shule hiyo kuporomoka kitaaluma.

Matukio ya kushambulia watumishi wa umma au binadamu mwingine ni lazima yakemewe, zipo njia za kisheria za kufuata kupata suluhu ya tatizo lililopo kuliko kutoa uhai wa mtu au kujeruhi yeyote.

Ni vyema hatua zikachukuliwa kuhakikisha uhusiano mwema unarejea katika kijiji hicho, kwa kufanya vikao vya mara kwa mara na mambo yanayoweza kuwaunganisha.

Bila kufanya hivyo bado kutaendelea kuwa na visasi kwa walimu na jamii hiyo, matokeo yake ushirikiano wa kuboresha kiwango cha taaluma utakuwa mgumu.

Kwa mujibu wa taratibu shule, kamati au bodi ambayo huundwa na wazazi, walimu na viongozi wa eneo hilo ni kusimamia maendeleo ya shule na kujenga ujirani mwema, hali inapokuwa tofauti ni lazima uhusiano wa pande hizo utayumba.

Uhusiano mwema ndiyo nguzo ya kuifanya shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma, ni wajibu wa jamii husika kurejesha hali ya amani na kuwa wa kwanza kufichua waliohusiana na mauaji hayo.

Vyombo vya habari vimetimiza wajibu wake wa kuisaidia jamii na matokeo yameonekana, kwa viongozi kuingilia kati ni ushahidi tosha kuwa kazi iliyofanywa inakwenda kutatua changamoto ya eneo hilo.

Huu utakuwa mwanzo wa kujenga uhusiano mwema baina ya pande zote na kuifanya shule hiyo kuandika historia na kuwa ya mfano wa ushirikiano wa kukuza taaluma.

Habari Kubwa