Uhusiano mzuri wa Tanzania na Rwanda ufungue njia kuendeleza watu wake

03Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Uhusiano mzuri wa Tanzania na Rwanda ufungue njia kuendeleza watu wake

TANZANIA kwa siku mbili ilikuwa na ugeni wa Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye alikuwa nchini kwa ziara ya siku mbili.

Ziara ya Rais Kagame, ambaye alitua nchini juzi na kuondoka jana, ya uhusiano mzuri baina ya mataifa haya mawili jirani.

Tanzania na Rwanda zimekuwa na uhusiano kwa kindugu kwa miaka mingi na tangu na pia tangu kuingia kwa uongozi wa awamu ya tano nchini mwetu chini ya Rais John Magufuli ushirikiano huu umeimarika zaidi.

Nchi hizi zimekuwa na uhusiano wa karibu kwa miaka mingi, kwa mfano pale yalipotokea matatizo ya kisiasa nchini Rwanda basi kimbilio lao mara nyingi lilikuwa Tanzania.

Ingawa katika miaka ya karibuni kuna wakati uhusiano kati ya nchi hizi mbili uliyumba kidogo na hata kutishia uhai wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini katika siku za karibuni hali imekuwa nzuri kutokana na kuwepo kwa mawasiliano mazuri kati ya nchi hizi mbili.

Ziara ya Rais Kagame imekuwa na manufaa mengi kutokana na makubaliano ya ushirikiano yaliyofikiwa kufuatia mazungumzo baina ya viongozi wa pande hizi mbili.

Ushirikiano huu umejikita zaidi katika kuongeza biashara baina ya mataifa haya mawili na uimarishaji wa miundo mbinu.

Hata hivyo, Tanzania, ambayo kwa sasa inajenga uchumi wake imeamua kujifunza baadhi ya mambo kutoka Rwanda.
Mathalani Serikali ya Rwanda imekubali kutoa wataalamu wake kuja kusaidia kushauri namna ya kufufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATC).

Pia Tanzania inatazamiwa kushirikiana na wataalamu kutoka Rwanda ili kuangalia uwezekano wa kuwa na akaunti moja ya fedha za umma.

Ni ishara nzuri kutokana na ukweli hatua hizi kwa kiasi kikubwa zitasaidia kwa kiasi kikubwa harakati za kujenga uchumi imara wa Tanzania.

Hata hivyo, tunatoa mwito wa kuimarishwa kwa uhusiano wa nchi hizi mbili na kuhakikisha kuwa hatua zinazochukuliwa zinagusa maendeleo ya watu wake.

Sote tunakumbuka kuwa Rwanda imepita katika kipindi kigumu na hasa yalipotokea mauaji ya kimbari mwaka 1993.

Hata hivyo, tangu mauaji hayo yalipozimwa mwaka 1994, nchi hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na kufanya mageuzi makubwa ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Nchi hiyo kwa sasa imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya tekinolojia na pia ni kivutio kikubwa cha uwekezaji.

Tunashauri kuwa kipaumbele cha ushirikiano wa nchi zetu uelekezwe zaidi katika maeneo, ambayo yatasaidia kuinua maisha ya wananchi wa nchi hizi mbili.

Kwa mfano tunapongeza hatua ya Serikali ya Tanzania ya kupunguza vizuizi vya barabarani wakati wa usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi nchini Rwanda.

Pia itakuwa jambo zuri ikiwa utafanyika upembuzi yakinifu ili kujua mahitaji ya nchi hizi mbili ili kuweza kufahamu maeneo ya kufanya biashara.

Kwa mfano, mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Iringa na Rukwa inajulikana kwa kuzalisha mahindi kwa wingi, kwa hiyo soko linaweza kupatikana Rwanda ikiwa kuna mahitaji ya zao hilo.

Pia Tanzania ina viwanda vya bidhaa mbalimbali, sasa linaweza kuangaliwa vizuri soko la nchi jirani ya Rwanda.

Tanzania pia ina mengi ya kunufaika kutoka Rwanda, ambayo katika miaka ya karibuni imepiga hatua kubwa likija suala la sayansi na tekinolojia.

Pia Rwanda imewekeza sana katika masuala ya sayansi na tekinolojia kwa mfano inashirikiana na Marekani katika kuendeleza wavumbuzi wake.

Taasisi kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inaweza kuangalia uwezekano wa namna ya kushirikiana na Rwanda katika kuendeleza wanasayansi wa kitanzania.

Kitu muhimu ni kuwa ushirikiano baina ya nchi hizi mbili ulenge zaidi katika kuendelea watu wa mataifa haya mawili.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa