Ukarabati wa shule za umma uungwe mkono

07May 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ukarabati wa shule za umma uungwe mkono

MIONGONI mwa sababu ambazo zimekuwa zikitajwa kuchangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini ni kukosekana kwa miundombinu rafiki katika shule zetu.

Hapa tunamaanisha uchakavu na uhaba wa majengo kama madarasa, mabweni, maktaba, ofisi za walimu na matundu ya vyoo. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa shule zetu nyingi za serikali.

Hali hii ilichangia kwa kiasi kikubwa mazingira ya wanafunzi kusomea na walimu kufundishia. Jibu la swali linaloweza kuulizwa ni kwamba ni kwa nini hali imekuwa hivi linaloweza kuwa ni kuwa hapakuwapo kipaumbele.

Hata hivyo, hali hiyo ni tofauti na miaka ya zamani ambapo elimu ilikuwa kipaumbele kikuu cha serikali kuanzia ukarabati, upangaji wa walimu wa kutosha katika shule pamoja na suala zima la ukaguzi wa shule.

Miaka ya baadaye kasi ya serikali ilishuka katika kusimamia na kuendesha shule zake na matokeo yake ni kuwa nyingi, hususan kongwe zikaporomoka kitaaluma (kufahaulisha), hivyo wazazi wengi hususan wenye uwezo kiuchumi kuanza kupeleka watoto wao katika shule za binafsi nje na ndani ya nchi.

Angalao baada ya serikali kuanzisha utaratibu wa kuzifanya baadhi ya shule zake kuwa za vipaji maalum katika miaka ya tisini, zilijaribu kubadili mtazano wa umma dhidi ya shule hizo, kutokana na kuongeza kiwango cha ufaulu. Hili linathibitishwa na matokeo ya shule hizo kama Mzumbe, Kibaha, Ilboru, Msalato, Kilakala, kwa kutaja baadhi kuwa mazuri na kushindana na shule bora za binafsi.

Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani ilianzisha utaratibu wa kuzikarabati shule zake kwa lengo la kuboresha kiwango cha elimu. Kwa kuanzia ilianza kutenga bajeti na kuanza kukarabati baadhi ya shule hizo.

Juzi Serikali ilisema kwamba imetenga zaidi ya Sh. bilioni 257 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe za Sekondari 89 nchini ambazo miundombinu yake ni chakavu.

Kwamba Lengo la hatua hiyo ni kuimarisha elimu na kuzifufua shule hizo ili ziweze kufanya vizuri kitaaluma kama ilivyokuwa zamani. Kati ya hizo katika mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18 tayari shule 46 zipo katika hatua mbalimbali za ukarabati wake.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, katika Kijiji cha Masanganya Kata ya Kibuta wilayani Kisarawe mkoani Pwani, alipokuwa akizindua madarasa mapya matatu na ukarabati wa madarasa mawili ujenzi uliofadhiliwa na Kampuni ya Yapi Merkez, inayojenga reli ya kisasa, ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji na huduma kwa jamii.

Jafo alisema Rais John Magufuli ameamua shule zote zikarabatiwe ili kuleta tija ya elimu nchini, na kwamba hii inaonyesha ni kwa kiasi gani Serikali inataka elimu iende mbele zaidi kwa kuwa kwa sasa kila mwezi zinatengwa Sh.bilioni 23.85 kwa ajili ya elimu bure kwa watoto wote wa shule za msingi na sekondari.

Kutokana na umuhimu mkubwa wa miundombinu rafiki mashuleni, tunaishauri serikali kuhakikisha fedha zaidi zinatengwa kwa ajili ya ukarabati wa shule zake, ili kuwawekea wanafunzi na walimu mazingira rafiki ya kusomea na kufundishia.

Uamuzi wa serikali wa kuzikarabati shule ni wa kupongeza kwa kuwa ni chachu katika suala zima la kuboresha elimu.

Hata hivyo, tunaelewa kuwa kazi ya ukarabati inahitaji fedha nyingi, lakini tunaamini inawezekana ikiwa utawekwa utaratibu mzuri na endelevu kwa kuishirikisha jamii na washirika wengine wa maendeleo.

Habari Kubwa