Ukosefu wa maji Hospitali ya Wilaya Bagamoyo ni aibu

21Apr 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ukosefu wa maji Hospitali ya Wilaya Bagamoyo ni aibu

KATIKA toleo letu la jana, tulichapisha habari ikieleza kwamba wauguzi wa wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, wanaosha mikono kwa kutumia maji ya dripu, kutokana na kukosekana huduma ya maji hospitalini hapo.

Hali hiyo inatokana mamlaka zinazohusika kuchelewesha ombi la hospitali hiyo la ununuzi wa tangi la kuhifadhia maji tangu Desemba, mwaka jana.

Kwamba ukosefu huo wa maji na uhaba wa mashine za kufulia mashuka, vimesababisha mazingira ya hospitali hiyo kuwa machafu.

Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Tumaini Bailon, alisema tatizo la maji linawapa wakati mgumu na kwamba tatizo hilo linasababisha mashuka kutofuliwa kwa wakati, huku wagonjwa na wauguzi nao wakikosa huduma hiyo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za usafi na tiba.

Kwa mujibu wa mganga huyo, kwa sasa wanapata maji kwa mgawo mara moja ama mara mbili kwa mwezi, huku tanki la maji linalotumika likiwa ni moja ambalo huwekewa maji baridi kwa ajili ya kufulia.

Dk. Bailon alibainisha changamoto nyingi zinazoikabili hospitali hiyo, lakini kinachoshangaza na kusikitisha ni kuona mamlaka husika zikichelewesha manunuzi ya vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

Hata kama kuna uhaba wa fedha, huduma ya maji safi na salama katika hospitali ni muhimu kuliko vitu vingine kwa kuwa hospitali ni taasisi inayopaswa kuwa mfano kwa hilo.

Kwa miezi kadhaa nchi yetu imekumbwa na ugonjwa hatari wa kipindupindu ambao imesababisha vifo vya watu kadhaa na wengine kulazwa hospitalini katika maeneo mengi nchini huku sababu inayosababisha hali hiyo ni uchafu ambao.

Maji yasiyo safi na salama ni sababu kubwa zinazochangia kipindupindu. Kama inafikia hatua kwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kukosa huduma ya maji na wauguzi kulazimika kutumia maji ya dripu, hilo ni tatizo na ni aibu kubwa kwa mamlaka zinazohusika.

Swali la kujiuliz ni je, serikali imekosa fedha za kunutulia tengi la maji kwa kipindi chote takribani miezi mitano sasa, au kuna maslahi bimafsi ya baadhi ya watu?

Wauguzi kutumia maji ya dripu kuosha mikono ni matumizi mabaya ya fedha za serikali kwa kuwa yananunuliwa kwa fedha nyingi, ni kukiuka maadili ya utabibu na ni kuchezea haki za wagonjwa.

Inashangaza kwamba hali hiyo inatokea wakati viongozi wa serikali wa kada mbalimbali katika wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Pwani hawachukui hatua zozote dhidi ya walioshindwa kutekeleza wajibu wao.

Tunawashauri viongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuingilia kati kwa kwenda haraka katika hospitali hiyo na kuweka mambo sawa.

Kama fedha hazijapelekwa basi zipelekwe harakakwa ajili ya kufanya nanunuzi ya matengi ya kuhifadhia maji, tiba na mambo mengine ili kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

Bila kuchukuliwa hatua za haraka itakuwa ni aibu kwa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imekuwa ikisisitiza kuwa lengo lake kubwa ni kuboresha huduma mbalimbali za jamii ikiwamo ya afya.

Ikumbukwe kwamba haiwezekani hospitali yoyote ikatoa huduma kwa wagonjwa bila kuwa na maji ya uhakika kwani kila kitu kinategema maji.