Ulipaji madeni ya serikali usiishie kwa makandarasi

09Feb 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Ulipaji madeni ya serikali usiishie kwa makandarasi

SERIKALI imewataka makandarasi waliosimamisha kazi za ujenzi wa miradi mbalimbali kurejea kazini, baada ya kuanza kuwalipa madai yao ya muda mrefu.

Serikali ya awamu ya nne kwa kipindi kirefu haikuwalipa makandarasi fedha zao kutokana na madai ya kutokuwa na fedha, hali iliyosababisha wengi wao kuondoka katika maeneo ya kazi na miradi mingi kukwama.

Katika Mkutano wa Bunge la Bajeti ya 2015/16 ilielezwa kwamba, Wizara ya Ujenzi ilikuwa inadaiwa na makandarasi zaidi ya Sh. bilioni 800 na kwamba ukijumlisha na riba, serikali ilikuwa inadaiwa takribani Sh. trilioni moja.

Hali hiyo ilisababisha miradi mingi kukwama hususani ya barabara ambayo ni kichocheo kikubwa katika ujenzi wa uchumi imara, kwani bila miundombinu ya barabara siyo rahisi kuwapo maendeleo.

Taarifa kwamba serikali ya awamu ya tano imeanza kulipa malimbikizo ya madai ya makandarasi zinatia moyo kwa kuwa hatua hiyo itawarejesha makandarasi katika maeneo ya ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwamo ya barabara na madaraja.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, amesema serikali imeshawalipa makandarasi waliosimamisha kazi Sh. bilioni 400 na kuwaomba warejee kazini na kuendelea na ujenzi.

Aliwataka makandarasi hao kuwapa mikataba ya ajira wafanyakazi wao katika kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa ili ujenzi wa barabara na madaraja ukamilike kwa mujibu wa mkataba.

Prof. Mbarawa ambaye alikuwa wilayani Mvomero, Morogoro kukagua ujenzi wa barabara ya Magole-Turiani yenye urefu wa kilomita 48.6, alisema licha ya serikali kuwalipa makandarasi kiasi hicho cha fedha, itaendelea kufanya hivyo ili kumaliza madeni yao haraka iwezekanavyo.

Kauli ya waziri huyo inaonyesha kwamba serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, hatua inazozichukua za kubana matumizi ya fedha za umma na kupambana na ufisadi zinasaidia kupatikana fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ni imani yetu kwamba mapato yanayopatikana kutokana na kuweka nidhamu katika matumizi ya serikali na kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi, yakielekezwa katika shughuli za maendeleo nchi yetu itapiga hatua kwa kasi kubwa.

Kama zimepatikana fedha zilizowalipa makandarasi ndani ya miezi mitatu ya uongozi wa awamu ya tano, kuna uwezekano mkubwa kwamba baada ya nusu ya uongozi wa Rais Magufuli hatua zinazoendelea kuchukuliwa zinaweza kuipaisha Tanzania kiuchumi.

Pamoja na kuanza kuwalipa makandarasi, serikali hainabudi pia kuweka utaratibu wa kuwalipa wadai wengine ambao wanaidai kwa muda mrefu na kulazimika kusitisha huduma. Kwa mfano, kuna wazabuni ambao wamekuwa wakitoa huduma kwa serikali na taasisi zake pamoja na watumishi wa umma.

Kulipa madeni hayo kutawaongezea imani wanaotoa huduma kwa serikali na kuwapa morali watumishi wa umma, wakiwamo walimu ambao wamekuwa wakidai stahiki zao mwa muda mrefu.

Hata hivyo, ushauri wetu ni kwamba serikali inapaswa kuwa makini katika mchakato wa ulipaji wa madeni ili kuepukana na uwezekani wa kuwapo kwa vitendo vya udanganyifu kwa baadhi ya wadai.

Serikali hainabudi kupitia kwa umakini nyaraka zote za madai ya malipo na kujiridhisha pasi na shaka kuwa wanaolipwa fedha hizo ni wadai halali na madai yao ni halali.

Habari Kubwa