Umakini unahitajika katika utekelezaji bajeti 2020/21

01Jul 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Umakini unahitajika katika utekelezaji bajeti 2020/21

BAJETI ya serikali kwa mwaka wa fedha 2020/21, inaanza kutekelezwa rasmi leo, serikali ikitarajiwa kukusanya na kutumia Sh. Sh. trilioni 34.88.

Katika bajeti hiyo ambayo ni ya mwisho kwa awamu ya kwanza ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, Sh. trilioni 21.98 zinatarajiwa kutumika kwa matumizi ya kawaida ukiwamo uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, huku Sh. trilioni 12.9 zikitarajiwa kutumika kwa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Leo, ikiwa ni siku ya kwanza kabisa ya kuanza kwa utekelezaji wa bajeti hiyo, Nipashe tunaikumbusha serikali umuhimu wa kuzingatia vipaumbele vilivyoanishwa katika bajeti hiyo.

Tunakumbusha vipaumbele hivyo vilivyowekwa katika viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, serikali ikitarajia kujenga viwanda vinavyotumia kwa wingi malighafi zinazopatikana nchini zikiwamo za kilimo, madini na gesi asilia, ili kukuza mnyororo wa thamani.

Katika hili, serikali iimeahidi kutekeleza miradi ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia, uanzishwaji na uendelezaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi na Kongane za Viwanda, viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuongeza thamani ya madini na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu.

Pia, kuweka mkazo katika kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo na zana za kilimo na uvuvi, huduma za ugani na utafiti, uimarishaji wa malambo na majosho, ujenzi wa maghala na upatikanaji wa masoko ya mazao na mifugo ndani na nje ya nchi.

Serikali pia imepanga kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na ujuzi na huduma za maji safi na salama kupitia utoaji wa elimumsingi bila ada, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuboresha huduma ya maji, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ununuzi na usambazaji wa dawa pamoja na ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya.

Nipashe tunakumbusha pia uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu nishati, usafirishaji pamoja na ununuzi na ukarabati wa ndege, meli na vivuko.

Mbali na vipaumbele hivyo, serikali pia inatarajiwa kupunguza tatizo la ajira nchini kwa kutoa ajira mpya kwa wananchi, hususan vijana waliohitimu vyuo vikuu na maeneo mengine ya kitaaluma.

Vilevile, tunakumbusha ahadi iliyotolewa ya kulipa madeni ya wazabuni, watumishi na mifuko ya hifadhi ya jamii ambako Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebainisha kuwapo kwa deni kubwa na la muda mrefu.

Ni katika mwaka huu wa fedha serikali kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA), itaanza kukusanya mapato yaliyokuwa yanakusanywa na mamlaka za kiuhifadhi likiwamo Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

Nipashe tunaona kuna haja mamlaka hizi zikakumbukwa na serikali kwa watumishi wake kulipwa mishahara na posho zao kwa wakati ili kuwa na motisha ya kazi sambamba na kutekeleza miradi ya mamlaka hizo kwa wakati ili kulinda hadhi ya utalii nchini.

Pia, Nipashe tunaamini kuwa, bila kuwapo kwa nidhamu katika matumizi, utekelezaji wa bajeti hiyo ya serikali hautafanikiwa, hivyo kuna haja serikali kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha utawala bora katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Ndiyo maana tunasisitiza mamlaka husika za serikali kuongeza umakini katika kuyatekeleza mambo haya muhimu yaliyopangwa kutekelezwa kwa mwaka huu wa fedha.

Habari Kubwa