Umakini utawale mradi wa mwendokasi awamu ya pili

07Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Umakini utawale mradi wa mwendokasi awamu ya pili

UTEKELEZAJI wa awamu ya pili  ya mradi wa mabasi yaendayo haraka utaanza jijini Dar es Salaam mwakani.

Mradi huo utajengwa kuanzia eneo la Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu na ujenzi huo utahusisha ulipaji wa fidia kwa wananchi ambao nyumba zao zitabomolewa kupisha ujenzi ambao utagharimu Sh. bilioni 360.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Ronald Rwakatare, alisema zabuni ya kumpata mkandarasi wa ujenzi huo inatarajiwa kutangazwa Januari mwakani.

Alisema kiasi hicho cha fedha kimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo na kati yake, zimo za kulipa fidia ambazo hata hivyo, hakuwa tayari kutaja kiasi halisi kilichotengwa kufidia wananchi watakaoathirika, kwa maelezo kuwa kazi ya uthamini haijakamilika.

Utekelezaji wa awamu ya pili utahitaji nyumba nyingi zivunjwe kwa kuwa unahusisha barabara ya urefu wa kilometa 19.3, na kutokana na hali hiyo, fidia kwa wananchi wanaomiliki nyumba katika maeneo yatakayoguswa na mradi huo haitaepukika.

Tunatiwa moyo na jitihada za serikali yetu za kuhakikisha miundombinu inaendelea kuboreshwa kwa kasi kubwa ili kutatua changamoto zilizokuwa zinajitokeza katika sekta ya usafiri na kukwaza shughuli za uchumi na kijamii.

Ulipaji wa fidia kwa wale ambao nyumba zao zitaathirika kwa namna moja au nyingine ni muhimu sana ili wapishe mradi na kwenda mahali pengine kuanza maisha mapya. Makazi ni moja ya haki za msingi kwa kila binadamu, hivyo inapotokea akayapoteza kwa sababu kadhaa ikiwamo hiyo, hanabudi kulipwa fidia kwa kuzingatia sheria na taratibu.

Hata hivyo, uzoefu wetu unaonyesha kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ambao unahitaji ubomoaji nyumba na kuchukuliwa ardhi na kuwalipa fidia wamiliki wake, umekuwa ikiibua mivutano baina ya  wananchi na mamlaka mbalimbali.

Kwa upande wake, serikali imekuwa ikisimamia sheria, taratibu na kanuni za ulipaji wa fidia na vile vile kufuata taarifa za tathmini ya maeneo husika na kuamua nani alipwe kiasi gani.

Hata hivyo, imekuwa ikiibuka mivutano kutokana na baadhi ya wananchi kutaka walipwe zaidi ya kiwango kilichowekwa na wathamini na kuibua malalamiko mengi na wakati mwingine baadhi yao kwenda mahakamani kuomba zuio la kusimamisha utekelezaji wa miradi husika.

Migogoro ya aina hii haina tija kwa kuwa imekuwa ni kikwazo katika jitihada na kasi ya  serikali katika  kuwaletea wananchi maendeleo.

Katika utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huu, tunawashauri wahusika wote kuhakikisha wanakuwa makini na kutumia busara ili mradi huo uanze na kukamilika kwa wakati, hivyo kutimiza lengo lake la kuondoa msongamano katika barabara za Jiji la Dar es Salaam.

Wananchi ambao nyumba zao zinapitiwa na mradi huo waondokane na tamaa ya kulipwa fedha zaidi za fidia kuliko wanazostahili kwa mujibu wa tathmini ya serikali. Watakaofanya vitendo vya kughushi nyaraka na ujanja mwingine wa kutaka kujipatia fedha kinyume cha sheria na taratibu watambue kuwa watauchelewesha mradi na kusababisha matatizo ya usafiri kuendelea kuwa kero.

Tunatoa angalizo pia kwa watumishi wa serikali wanaohusika katika zoezi la tathmini ya nyumba zitakazobomolewa pamoja na watendaji wa  kata na mitaa kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa lengo la  kujinufaisha, badala yake wazingatie uadilifu na weledi ili haki itendeke.

Wananchi, watendaji na watumishi wote wanapaswa kuelewa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo ni mkopo wa Benki ya Dunia kwa serikali, na baadaye zitatakiwa kurejeshwa. 

Habari Kubwa