Umuhimu NHC bado ni mkubwa

24Oct 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Umuhimu NHC bado ni mkubwa

WABUNGE wamenusu harufu ya kukwama kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kueleza mambo mengi yanayoonyesha kuwa hatima ya taasisi hiyo ya umma, si njema.

Kabla ya kuanza kuibana NHC, tunakubaliana kama taifa kuwa, nchi kuwa na shirika hilo ni njia mojawapo ya kujenga miji na kuifanya ya kisasa zaidi kupitia uwekezaji kwenye majengo na ardhi.

Pamoja na kasoro zinazoibuliwa kuhusu NHC kuwa na urasimu na kushindwa kutoa ripoti za taarifa zake na utendaji kazi, wengi tunakubaliana kuwa shirika la umma kama hilo bado lina nafasi kubwa kwenye uwekezaji.

Ndilo linaloweza kuleta makazi bora kwa watu wasio na kipato, wenye kipato cha kati, kikubwa, vitega uchumi, ofisi na pia maeneo ya burudani kama hoteli.

Lakini pia, tunakubaliana kuwa uwekezaji huo ni wa gharama kubwa ambao faida zake haziwezi kuonekana kwa muda mfupi na hii ndiyo hatari zaidi iwapo miradi ya NHC na usimamizi wake utafanyika bila uadilifu.

Tunakumbusha kuwa faida za taasisi kama NHC ni zile zinazopatikana baada ya muda mrefu mno kwa hiyo si lelemama.

Ni wazi kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ina hoja za msingi ambazo NHC inatakiwa kuzijibu na kuzifanyia kazi.

Ila pamoja na kuufuatilia ushauri wa PAC tunatoa angalizo kuwa uwekezaji kwenye majengo na ardhi (estates) ni mambo ya gharama kubwa mno ambayo faida zake huja baada ya miongo mingi hata zaidi ya mitatu lakini bila umakini unaweza usipatikane pia.

Hii ni kwa sababu eneo hili ni tofauti na masoko ya mitaji na fedha, dhamana au hati fungani za serikali.

Ndiyo maana ili shirika kama NHC liwe na tija ni lazima kuwa na uadilifu na uaminifu kwani kazi zake zinaweza pia kuhusisha, kununua ardhi, kufidia wamiliki, mikopo ya ujenzi na gharama za ununuzi wa vifaa na ujenzi.

Ni wazi kuwa nyakati nyingine nyumba hizo zinahitaji kufanyiwa matengenezo, uangalizi na usimamizi wa kudumu ili ziendelee kuwa na tija na kuzalisha zaidi katika nyakati zilizopo na siku zijazo.

Hata hivyo, kama taifa, ili shirika la NHC lianze kuleta faidi ni lazima kuhakikisha kuwa linakuwa na mtaji wa kutosha pamoja na uwekezaji mpana pia.

Aidha, katika mipango mojawapo ni kutekeleza jukumu la kujenga na kuuza nyumba au majengo yake kwa watu wa aina mbalimbali.

Lakini, ni lazima NHC ijiendeshe kwa tija tena iwe chanzo cha mapato. Kama tulivyosema kwa kujenga nyumba na kuzikodisha wengine ambao wanazitumia kufanyabiashara.

Kwa mfano, kumilika majengo ambayo hutumiwa kama hoteli, hospitali, mabweni (hosteli) au kumbi za mikutano.

Ili haya yafanikiwe ni lazima kuwa na ardhi, mtaji, wataalamu na wajuzi wa kutumia ardhi na majengo hayo kwa faida, lakini pia utambuzi wa wateja wa kimkakati kile kinachohitajika kwenye soko la nyumba kwa wakati huo.

Ripoti ya Benki ya Dunia ya Africa’s Cities ya mwaka 2017, ilitaja bayana kuwa Afrika inakabiliwa na ongezeko kubwa la watu mijini lisiloendana na kasi ya huduma za makazi.

Aidha, inaeleza kuwa majiji ya Afrika Dar es Salaam na Dodoma zikiwamo hayana majengo makubwa wala ofisa kutosha.

Kwa kuangalia ripoti hiyo, tunaona kuwa NHC ni muhimu mno zama hizi katika kujenga majengo ya aina mbalimbali.

Kwa hiyo umuhimu wa shirika la nyumba kama hilo ni mkubwa katika mazingira ya sasa yanayohitaji uwekezaji kwenye majengo kwa ajili ya makazi na vitega uchumi.

Ripoti ya Benki ya Dunia ya Africa’s Cities ya mwaka 2017, ilitaja bayana kuwa Afrika inakabiliwa na ongezeko kubwa la watu mijini lisiloendana na kasi ya huduma za makazi.

Aidha, inaeleza kuwa majiji ya Afrika Dar es Salaam na Dodoma zikiwamo hayana majengo makubwa wala ofisa kutosha.

Kwa kuangalia ripoti hiyo, tunaona kuwa NHC ni muhimu mno zama hizi katika kujenga majengo ya aina mbalimbali.

Kwa hiyo umuhimu wa shirika la nyumba kama hilo ni mkubwa katika mazingira ya sasa yanayohitaji uwekezaji kwenye majengo kwa ajili ya makazi na vitega uchumi.

Habari Kubwa