Upo umuhimu serikali, wanahabari kuzungumza

04May 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Upo umuhimu serikali, wanahabari kuzungumza

APRILI 16, mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alitoa kauli iliyoleta matumaini makubwa kwa vyombo vya habari, baada ya kuagiza vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe.

Hata hivyo, alivitaka vyombo hivyo vifuate taratibu na sheria katika kufanyakazi zao.

Kwa mujibu wa takwimu zilizonukuliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini, sio ya kuridhisha kutokana na kuporomoka viwango vya kimataifa kutoka nafasi ya 71 mwaka 2016 hadi nafasi ya 124 mwaka 2020.

Hali ya kufungiwa kwa baadhi ya magazeti na televisheni mtandao, imekuwa ikilalamikiwa na wadau wa habari kwa kubinywa kwa uhuru wa vyombo vya habari na kunyima wananchi haki ya kupata habari.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yaliyofanyika jana kitaifa jijini Arusha, amempongea Rais Samia kwa hatua yake ya kuagiza vyombo hivyo kufunguliwa kwa kuwa imeleta nuru mpya.

Kufungiwa kwa magazeti na kufunguliwa kesi za jinai, waandishi wa habari kupigwa na kunyang'anywa baadhi ya vifaa vya kazi na wengine kupotea ni matukio ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wadau wa vyombo vya habari kutofanyakazi yao kwa uhuru.

Vyombo vya habari kwa kutoandika habari za kuibua masuala kuleta mabadiliko katika nchini, kulipoteza dhana nzima ya vyombo hivyo katika kuzingatia misingi na weledi wa taaluma yao kuisaidia serikali kutekeleza majukumu yake katika utawala bora.

TEF imeomba watawala kuheshimu uhuru wa habari na kufanya kazi kwa ushirikiano na wanahabari na kufuatilia kwa karibu matukio ya wanaofungia wanahabari na vyombo vyake ili kuwadhibiti watu wachache wanaoendelea kuharibu dhamira njema ya serikali.

Tunaanza kuona matumaini mapya baada ya serikali kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, inakaribisha mazungumzo pale vyombo vya habari vinapoona mambo hayaendi sawa ili kila mmoja afanye kazi kwa uhuru.

Na kwamba serikali itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari pamoja na wadau wa habari nchini kwa ajili ya kuendelea kuelimisha jamii mambo mbalimbali yenye tija kwa taifa.

Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kutoka Canada, Uingereza na Marekani wamepongeza pia hatua iliyoanza kuoneshwa na Rais Samia katika kuleta mabadiliko ya uhuru wa vyombo vya habari.

Hata hivyo, wamevitaka vyombo vya habari kuandika habari zenye uhakika, kuaminika na zinazotoka haki pande zote ili wananchi waweze kujenga imani kwa vyombo hivyo.

Katika maadhimisho hayo, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Tirso Dos Santos, alisema shirika hilo limekuwa likisaidia taaluma ya habari katika nyanja mbalimbali nchini, kwa kuwajengea uwezo wanawake viongozi katika sekta ya habari.

Alisema licha ya kujengea uwezo wanawake, mwaka jana wametumia zaidi ya Sh. milioni 400 kwa ajili ya kununua vifaa vya redio 16 za kijamii nchini lengo likiwa kuhakikisha jamii inapata habari kwa wakati.

Ni imani yetu kuwa ushirikiano wa vyombo vya habari, serikali na wadau wa habari utaleta mafanikio makubwa katika kuhabarisha umma na kuleta mabadiliko ya kiuchumi.

Habari Kubwa