Urasimishaji wa vijiji hifadhini umakini muhimu

17Jan 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Urasimishaji wa vijiji hifadhini umakini muhimu

MOJA ya changamoto ambazo zimekuwa zikizua migogoro ya mara kwa mara kati ya mamlaka za serikali na wananchi ni wananchi kudaiwa kuvamia na kuishi katika maeneo ya hifadhi.

Hali hiyo imekuwa ikisababisha serikali itumie nguvu kuwaondoa kwa maelezo kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria za hifadhi za taifa, mapori tengefu na mapori ya akiba.

Matumizi ya nguvu za dola yamekuwa yakihusisha pia kuwaondoa wananchi hao, kuwashtaki katika vyombo vya sheria, kuharibu mazao yao na wakati mwingine kukamata na kutaifisha mifugo yao.

Oparesheni kadhaa zilizowahi kufanywa na mamlaka za serikali ikiwamo ‘Tokomeza’ ziliwaathiri wananchi wengi waliokutwa wakiishi katika maeneo ya hifadhi kwa kuhusishwa na vitendo vya ujangili.

Wako wananchi ambao waliuawa, kupata vilema, kuharibiwa mali na nyingine kupotea ikiwamo mifugo katika operesheni hiyo iliyotekelezwa na kikosi kazi maalum.

Licha ya kamati ya uchunguzi ya Bunge kufichua madhila ya operesheni hiyo na baadhi ya watumishi wa umma kuchukuliwa hatua wakiwamo mawaziri waliowajibika kwa kujiuzulu, bado suala la wananchi kuvamia na kuishi hifadhini kimekuwa likiendelea kuigonganisha serikali na wananchi.

Takribani wiki iliyopita mawaziri kadhaa walitembelea mkoa wa Kigoma na kuazimia kufanyika kwa operesheni ya kitaifa ya kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo ya hifadhi na kufanya shughuli za kibinadamu.

Hata hivyo, juzi Rais John Magufuli alifanya uamuzi, ambao unaonekana kuwa ni kutatua kero wanazozipata wananchi hao.

Rais aliagiza kusitishwa mara moja kazi ya kuviondoa vijiji na vitongoji vinavyodaiwa kuwa kwenye maeneo ya hifadhi na amewataka viongozi wa wizara zote zinazohusika kukutana ili kubainisha na kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo ya vijiji na vitongoji hivyo.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo Ikulu jijini Dar es Saalam alipokutana na viongozi wakuu wa wizara zinazohusika na masuala ya ardhi.

Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli aliwataka viongozi wa wizara husika kubainisha maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu ambayo hayana wanyamapori au misitu ili yagawiwe kwa wafugaji na wakulima.

Rais aliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia upya kazi ya uwekaji wa mipaka ya hifadhi na makazi na kutumia busara katika uwekaji wa mawe ya mipaka hiyo ili kutowaondoa wananchi katika maeneo ambayo hayana ulazima wa kuwaondoa.

Vile vile, aliagiza vijiji vyote 366 vilivyoainishwa kuwapo ndani ya maeneo ya hifadhi nchini, visiondolewe katika maeneo hayo. Badala yake, alitoa mwezi mmoja kwa viongozi wa wizara zote zinazohusika kubainisha maeneo ya vijiji hivyo na kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya sheria ili yawasilishwe katika kikao kijacho cha Bunge.

Uamuzi huo ni wa msingi kwa kuwa unazingatia mahitaji halisi ya wakulima na wafugaji ambao wanahitaji maeneo kwa ajili ya malisho na kilimo, kwa kuzingatia kuwa kadiri miaka inavyoenda idadi ya watu inaongezeka, hivyo lazima iendane na mahitaji na matumizi ya ardhi.

Jambo la msingi, tunawashauri kazi ya kuyarasimisha maeneo hayo yafanyike kwa umakini mkubwa kwa lengo la kuepusha athari nyingine zinazoweza kuibuka baadaye.

Tinasema hivyo kwa kuwa mara nyingi tumeshuhudia utekelezaji wa maagizo kuhusu masuala yanayowagusa wananchi ukizua malalamiko na migogoro kutokana na watendaji kukosa umakini.

Habari Kubwa