Usafiri bure walimu Dar iwe hiari ya wasafirishaji

02Mar 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Usafiri bure walimu Dar iwe hiari ya wasafirishaji

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni na viongozi wa vyama vya usafirishaji abiria jijini Dar es Salaam, wamekubaliana kuwa walimu wa shule za msingi na sekondari za serikali kuanzia Machi 7, mwaka huu, wasilipe nauli katika daladala.

Utekelezaji wa makubaliano hayo utaanza utaanza baada ya kukamilika utengenezaji wa vitambulisho maalum kwa waalimu hao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabruki, alisema makubaliano hayo ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Magufuli katika kutekeleza mpango wa elimu bure na kupunguza makali ya maisha kwa walimu hao.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, walimu wataanza kusafiri bure kuanzia saa 11:30 alfajiri hadi saa 2:00 asubuhi, na saa 9:00 alasiri hadi saa 11:00 jioni. Nje ya muda huo, alisema watalazimika kujilipia na walimu wote watasafirishwa kwa utaratibu wa vitambulisho pamoja na kuwapo na utaratibu wa kila gari kuingia walimu wachache.

Tunawapongeza Makonda na viongozi wa Darcoboa kwa kufikia makubaliano hayo kwa lengo la kuunga mkono mpango ulioanzishwa na Rais Magufuli wa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wameeleza changamoto kadhaa ambazo zinaweza kukwamisha makubaliano hayo.
Kwa mfano, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimesema kinahitaji kuwapo kwa mkataba wa kimaandishi kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Darcoboa kwa hofu kwamba suala hilo linaweza likawa la kisiasa zaidi.

Kadhalika, CWT inaeleza kuwa kama serikali imedhamiria kuwasaidia walimu, inapaswa kupeleka mkakati huo hata kwa walimu wa mikoa yote na kuhakikisha walimu hawanyanyapaliwi kama wanafunzi wanavyonyanyaswa kwenye mabasi.

Suala lingine ambalo linazua shaka kuhusiana na utekelezaji wa mpango huo ni kwamba pamoja na wamiliki wa daladala kukubali kuwasafirisha walimu bure, lakini wanaosimamia magari yao ni madereva na makondakta, ambao mapato yao hutokana na nauli zinazolipwa na abiria.

Madereva na makondakta wa daladala wana mikataba na wamiliki ambayo inawataka kuwasilisha kiasi fulani cha mapato ya siku kwa tajiri na kinachobaki ndicho wanachokichukua. Katika mazingira magumu ambayo makondakta na maderava wanapata fedha zao, kuna ugumu kuwaruhusu walimu wasafiri bila kulipa nauli.

Uzoefu wetu umetuonyesha kwamba madereva na makondakta wamekuwa wakikataa kuwasafirisha wanafunzi ambao wanatakiwa kulipa nusu ya nauli ya mtu mzima na pale wanapowasafirisha huwanyanyasa.

Hata polisi na wanajeshi ambao husafiri kwenye daladala bila kulipa nauli, hawanyanyaswi na makondakta na madereva kwa kuwaogopa na si vinginevyo.

Kasoro nyingine ambayo inaweza kukwamisha utekelezaji wa makubaliano hayo ni kutokana na kutowashirikisha madereva kupitia Chama cha Madereva wa Daladala Dar es Salaam (Uwadar).

Kama wangeshirikishwa katika kabla ya kufikia makubaliano hayo na kukubali kwa hiyari yao kuwasafirisha walimu bure, pasingekuwapo shaka yoyote kuhusiana na utekelezaji wake.

Kadhalika, wapo wamiliki wa daladala ambao siyo wanachama wa Darcoboa. Inawezekana wasiwe tayari kukubaliana na mpango huo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ya kulipa kodi nyingi za serikali.

Kutokana na hali hiyo, tunashauri kwamba njia shirikishi ya wadau hao ingetumika kabla ya kufikia makubaliano baina ya serikali na Darcoboa ili uamuzi huo uwe wa hiari.

Habari Kubwa