Usajili huu Simba, Yanga uzingatie michuano Caf

24Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Usajili huu Simba, Yanga uzingatie michuano Caf

JUMAPILI wiki hii Juni 30, ndiyo siku ambayo klabu zinazowakilisha nchi zao kwenye michuano ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika zinatakiwa ziwe zimekamilisha usajili wao.

Hiyo ni kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), na tayari klabu husika hususan hapa nchini, Simba, Yanga,  Azam FC na KMC zimekuwa katika mchakato wa kuimarisha vikosi vyao kuelekea michuano hiyo.

Ikumbukwe, Simba na Yanga zitaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa wakati Azam na KMC zenyewe zikitakiwa kuhakikisha bendera ya Tanzania kwa upande Bara inapepea vema kwenye kitimtimu cha Kombe la Shirikisho Afrika.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya soka la Tanzania Bara, kuwakilishwa na timu nne kwenye michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu Afrika. Hivyo ni matarajio ya Nipashe kuona wawakilishi hao wa Tanzania Bara wakifanya usajili makini utakaowawezesha kufika mbali kwenye michuano hiyo na kuwa sehemu ya zitakazonufaika na utajiri huo.

Kama inavyofahamika, bingwa wa michuano hiyo huibuka na dola za Kimarekani milioni 2.5 (Sh. bilioni 5.7), huku mshindi wa pili akizawadiwa dola milioni 1.25 (Sh. bilioni 2.8 za Tanzania).

Na si bingwa na mshindi wa pili tu ambaye huibuka na donge hilo nono,  bali pia timu inayotinga nusu fainali huibuka dola 800,000 (Sh. bilioni 1.8) na robo fainali huzawadiwa dola 650,000 (Sh. bilioni 1.5), huku timu zinazoshika nafasi ya tatu na ya nne kwenye hatua ya makundi zikinufaika na utajiri huo wa Caf kwa kupewa dola 550,000 (Sh. bilioni 1.2).

Ndiyo maana tunatamani kuona wawakilishi wetu wakiongeza umakini zaidi katika kusainisha wachezaji kwa kutazama wenye sifa na viwango vya kutoa ushindani kwenye michuano hiyo.

Kwa miaka mingi Simba na Yanga zimekuwa na utamaduni wa kusainisha wachezaji kwa sifa ama kukomoana zenyewe kwa zenyewe, huku zikiwa hazizingatii mapendekezo ya makocha wao na matokeo ya usajili kama huo ni kocha kuchukua muda mrefu katika kukiandaa kikosi chake kwa kuweza kupata 'kombinesheni' inayoweza kumpa ushindi.

Aidha, wasiwasi wetu pia ni namna klabu mfano Yanga inavyosainisha wachezaji wengi, hiyo ikiwa ni dalili ya mabadiliko makubwa ambayo pia yatamchukua kocha muda mrefu kuweza kupata kikosi imara cha kwanza.

Nipashe tukiwa kama wadau na wazoefu wa michezo hususan soka, tulitarajia kuona wawakilishi wetu hao wakiziba mapengo na kuimarisha idara ambazo zilipwaya msimu uliopita na si kusainisha karibu kikosi kizima cha kwanza. Wawakilishi wetu hawana budi kutambua kuwa michuano wanayokwenda kushiriki ni mikubwa na migumu na inahitaji ubora wa mchezaji mmoja mmoja, lakini pia kucheza kitimu.

Simba msimu uliomalizika ilifanikiwa kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kilichoisaidia ni kuweza kucheza kitimu zaidi kwani wapinzani wao licha ya kucheza kitimu walikuwa bora zaidi kwa upande wa uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja.

Ni wazi kwa klabu zetu hazina uwezo kifedha kushindana sokoni katika kuwania wachezaji bora na klabu kama Al Ahly, Esperance ama TP Mazembe, hivyo kinachoweza kuzibeba katika michuano hiyo ni kucheza kitimu zaidi, jambo ambalo linahitaji wachezaji kucheza kwa pamoja muda mrefu ili kuzoeana.

Pamoja na hilo, basi usajili huo hauna budi kumulikwa kwa kutazama wachezaji ambao wanaweza kuzibeba timu kwa uwezo wao binafsi badala ya kufanyika kwa mihemko zaidi kama tunavyoshuhudia kwa sasa.

Habari Kubwa