Usajili wa Vicoba usimamiwe vizuri

25Feb 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Usajili wa Vicoba usimamiwe vizuri

JUZI Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilifafanua na kutoa msimamo wa tozo na kodi ambazo zinasemekana kuwa zitatozwa kwenye vikundi vidogo vidogo yaani Vicoba.

Ufafanuzi huo umetolewa ukiwa umebaki mwezi mmoja na siku nne kufika tarehe ya mwisho ya usajili wa taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha, taasisi zinazotoa mikopo bila kupokea amana za umma ikijumuisha kampuni za kukopesha, kutoa huduma ndogo kwa njia za kidijitali na watu binafsi wanaokopesha.
 
Wengine ni vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na Vicoba. Aidha, sheria imebainisha kuwa benki zinazofaya biashara ya huduma ndogo za benki na huduma ndogo za fedha zitasimamiwa kwa mujibu wa sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
 
Jukumu la kisheria la BoT ni kusimamia na kufuatilia, kutunga kanuni na kusimamia watoa huduma, lakini sheria imetoa mwanya wa kukasimisha mamlaka na majukumu yake ya kutoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali.
 
SACCOS zinasimamiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na VICOBA ni mamlaka za serikali za mitaa ambazo ni halmashauri na manispaa.
 
Aidha, BoT ilieleza imesikia malalamiko ya wananchi kutozwa fedha kwa ajili ya usajili ambao bado haujaanza kwa kuwa ilisubiri mwongozo, kukamilika kwa mfumo wa usajili na elimu kwa maofisa maendeleo ya jamii.
 
Tayari mifumo imekamilika na mafunzo kwa maofisa maendeleo ya jamii, ambao sasa wanawajibika kutangaza kuanza usajili kwenye maeneo yao na ndani ya siku 14 vikundi viwe vimepata usajili.
 
Mwongozo uko bayana na kanuni zimefafanua kila kitu ni wajibu wa maofisa maendeleo ya jamii kufikisha elimu kwa umma ili kuondoa mkanganyiko uliokuwapo kuwa kuna kodi zitakazotozwa kwenye fedha za wanakikundi kwa mwezi na mwisho wa mwaka faida nayo itatozwa kodi.
 
Hali hiyo imesababisha baadhi ya vikundi kuanza kuweka fedha nyumbani na kuachana na utaratibu rasmi wa kwenda benki, huku wengine wakivunja vikundi kwa madai kuwa fedha zao zitatozwa kodi kubwa.
 
Baadhi ya vikundi vilijikuta chini ya baadhi ya SACCOS na wadhamini ili kukimbizana na usajili, ambako huko walitozwa fedha za usajili, jambo ambalo BoT imelipinga na kutaka watu kupata taarifa sahihi kutoka sehemu sahihi.
 
Ni matumani yetu kuwa baada ya maofisa maendeleo ya jamii kuelimishwa watafikisha elimu kwa wananchi na vikundi vinavyofika kwenye ofisi zao kwa ajili ya usajili, kwa kuwa kumekuwa na vikwazo vingi katika kusajili.
 
Kama ambavyo BoT inasisitiza kuwa hakuna tozo zozote zinazofanywa na mamlaka yoyote katika usajili, tunatarajia halmashauri zitasimamia kwa ufasaha kuhakikisha kuwa vikundi havikatishwi tamaa kwa sababu ambazo hazipo au kutozwa fedha ambazo kimsingi hazistahili.
 
Ni matarajio yetu kuwa TAMISEMI na madiwani watafuatilia kwa kina suala hili, ili kuondoa usumbufu ambao vikundi vinaupata na mwisho kujiendesha kwa siri au kuvunja vikundi ambavyo viliwakwamua wengi kimaendeleo.
 

Habari Kubwa