Usajili wa wachezaji waachiwe makocha

02Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Usajili wa wachezaji waachiwe makocha

HIVI sasa klabu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara, ligi daraja la kwanza zipo kwenye haraka za kusajili wachezaji wapya ili kuimarisha vikosi tayari kwa msimu ujao.

Ligi ambayo ilimalizika mwezi uliopita kwa Simba kutwaa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo, sasa inazipa nafasi za klabu kujipanga kwa ajili ya msimu mpya.

Timu nne zitawakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, hivyo usajili wa wachezaji muhimu zaidi kwa ajili ya kuboresha vikosi vyao.

Na sasa timu zimeingia kwenye vita ya usajili ingawa tayari kuna nyingine zilishaanza kusajili mapema tu na hii ni kutokana na ligi ya msimu huu kuchelewa kuisha sababu ya janga la Corona.

Tumeshaanza kuona viongozi wa timu kadhaa hapa nchini wakisafiri kwenda nje ya nchi kufuatilia wachezaji na shughuli nyingine za kitimu.

Wakati timu zinaenda kwenye vita ya usajili zinapaswa kukumbushwa kuwa, zinatakiwa kusajili kulingana na upungufu na siyo kusajili kwa sifa kisa zimeona timu zingine zinafanya hivyo.

Msimu uliopita tulishuhudia sajili nyingi sana na wachezaji baadhi walikuwa wakipokelewa kwa makundi makubwa ya mashabiki wa timu husika hivyo basi, Nipashe tunaona viongozi wayaachie kazi mabenchi ya ufundi yafanye kazi yao na wao wabaki kwenye suala la kutoa fedha ili kukamilisha usajili.

Makocha wanatakiwa wasiingiliwe linapokuja suala la kiufundi, maana ndiyo kazi waliyosomea na viongozi wadili na suala la kiutawala na kuingilia majukumu yasiyomuhusu.

Kocha anatakiwa kuachwa afanye usajili wa wachezaji anaowataka na hata ikitokea wakashindwa kufanya vizuri basi anapotimuliwa kazi, basi iwe kwa haki, kwamba kwa kuwa mlimpa kila alichokihitaji na yeye akashindwa kuwapa furaha, basi hakuna budi kumwondoa, hapo hamna dhambi kabisa maana kila upande umetenda haki.

Viongozi msisajili wachezaji ambao mwisho wa siku wanaishia kukaa benchi au jukwaani.

Tumeona wachezaji wakali wakitoka huko timu za kawaida wanaenda timu kubwa wakiwa na viwango vya juu, lakini huko wanakutana na wakubwa zaidi yao na kujikuta akiishia benchi na kuua vipaji vyao.

Au kiongozi utaona anasajili tu mchezaji ilimradi anajua anapata asilimia kumi wao huita ‘ten percent’ sasa hii inakuwa inaharibu soka, sawa inawezekana wakati mwingine kamali inakubali kwa mchezaji kuwika kwa kuwa msaada lakini mara nyingi huwa wanafeli.

Tunajua kwamba, sasa hivi wachezaji wengi wanaangalia fedha, lakini ni bora ukakaa sehemu ambayo unafanya kazi yako kwa amani bila presha na unalipwa kama kawaida hata kama ni fedha ya kawaida kuliko kwenda sehemu ambayo unalipwa sana, huchezi hata benchi hukai unaishia jukwaani, hapa unaua kipaji.

Ili soko liweze kuonekana inatakiwa uonekane unacheza sasa kama umekubali kulipwa fedha nyingi na unaenda kuishia kukaa jukwaani ni kazi bure.

Makocha nao msikubali tu kupelekwa na viongozi wakati mkijia fika kuwa nyinyi ndio wataalamu wa benchi la ufundi na mnajua wachezaji gani wanaofaa kwenye kikosi chako.

Kazi ya kocha ni kupendekeza majina ya wachezaji anaowahitaji na ambao anaona wanaweza kuwa msaada kwa timu, na hivyo mkiwaachia viongozi wawasajilie wachezaji, mzigo baadaye unaangukia kwenu.

Hivyo basi, Nipashe tunaona kwamba, makocha wasiingiliwe kwenye kazi ya usajili ili waweze kupata nyota wazuri ambao wataweza kuisaidia timu.

Habari Kubwa