Usajili Yanga, Azam umulike Simba ilipoteleza kimataifa

28Jun 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Usajili Yanga, Azam umulike Simba ilipoteleza kimataifa

NI rasmi Simba, Yanga na Azam zitaiwakilisha Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa kwa msimu mpya wa 2021/22 unaotarajiwa kuanza mapema Septemba, mwaka huu kwa mechi za hatua ya awali Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kupigwa.

Msimu huu Tanzania Bara itaingiza timu nne; mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho Afrika, nafasi hizo zikitokana na juhudi za Simba kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, hivyo kuiongezea nchi pointi na kuwa miongoni mwa nchi 12 zinazoruhusiwa kuingiza idadi hiyo kwa msimu.

Kwa mujibu wa Kanuni za Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bingwa wa Tanzania Bara na mshindi wa pili atacheza Ligi ya Mabingwa, huku mshindi wa tatu na Bingwa wa Kombe la FA wakicheza Kombe la Shirikisho.

Lakini endapo ikitokea Bingwa wa Ligi Kuu, akatwaa tena ubingwa wa Kombe la FA, basi mshindi wa tatu na wa nne wa Ligi Kuu ndiyo watakaokwenda kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Hivyo, kwa namna msimamo wa Ligi Kuu ulivyo hadi sasa, Simba ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo, huku Yanga na Azam zikiwa tayari zimejihakikishia kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kutokana pointi zilizonazo kutoweza kufikiwa na timu yoyote zilizopo nyuma yao.

Lakini pia Simba na Yanga zimetinga fainali ya Kombe la FA, hivyo hiyo ni tiketi ya wazi kabisa kwa timu mojawapo itakayoibuka mshindi kushiriki michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani humu, inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika, CAF.

Ingawa bado msimu wa 2020/21 haujamalizika huku dirisha rasmi la usajili likiwa pia halijafunguliwa, tayari klabu za Yanga na Azam FC zimeanza kuingia mikataba ya awali na wachezaji wapya, na kwa sasa zikisubiri tu dirisha hilo kufunguliwa ili kusajili mikata yao TFF.

Kwa ujumla tunazisifu kwa kuchukua hatua mapema kwani tunaamini hadi kufikia hatua hii zikiwa zimebakiza takriban michezo mitatu kabla ya msimu kumalizika, zimeshaelewa maeneo ambayo zinapaswa kuyaboresha katika Vikosi vyao.

Lakini hatuna budi pia kuziasa kuwa makini zaidi katika mchakato huo wa usajili kutokana na majukumu makubwa ya michuano ya kimataifa yaliyopo mbele yao kuelekea msimu mpya utakaoanza Septemba, mwaka huu.

Ni wazi kwamba Yanga na Azam FC zilishuhudia namna Simba ilivyopambana katika michuano hiyo na upinzani mkubwa iliyoupata, hivyo kwa kuanzia kama kweli zimedhamiria kufika mbali, zinapaswa kusajili wachezaji wenye uwezo kama ama zaidi ya wapinzani wao hao.

Hakuna ubishi kwamba Simba kwa sasa nchini ni klabu pekee inayojengwa na wachezaji wenye viwango vya juu zaidi, lakini bado haikufanikiwa kupenya nusu fainali na hatimaye fainali, hivyo kipimo cha usajili kwa Yanga na Azam kuelekea michuano hiyo kinapaswa kuwa ama daraja la wachezaji wa sasa wa Simba au zaidi ya hapo.

Tunatambua kwamba kuzidiwa mbinu ndiko kulikoifanya Simba kuishia robo fainali na si suala la uwezo wa wachezaji pekee, ndiyo maana tunawataka wawakilishi wetu hao wa msimu ujao kuhakikisha wanasajili wachezaji wa daraja la juu zaidi wakati huu pia Simba nayo ikitakiwa kujiimarisha kwa kuongeza nyota wenye uwezo zaidi ya walionao.

Kadhalika, kuna uwezekano mkubwa kwa Biashara United ya Mara kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo ya CAF kutokana na pointi ilizo nazo kwenye msimamo wa Ligi Kuu katika nafasi ya nne waliyopo, hivyo nayo haina budi kuanza kumulika wachezaji wa daraja la juu, kwani lengo letu ni kutaka kuona msimu huu timu zote nne zinatinga hatua ya robo fainali ama zaidi ya hapo kwenye mashindano hayo ili kujikusanyia pointi nyingi zaidi na kushikilia nafasi yetu ya timu nne.

Habari Kubwa