Usalama wa chakula sasa uwe kipaumbele

28Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Usalama wa chakula sasa uwe kipaumbele

LEO mkutano wa awali wa Umoja wa Mataifa kujadili mifumo salama ya kuzalisha chakula duniani, unahitimishwa, jijini Roma Italia ukiwa umeangazia mambo mbalimbali yanayohusu usalama wa chakula.

Katika mkutano huo mnyororo mzima wa kuzalisha chakula kuanzia mazao shambani, mifugo, samaki majini, hadi usaafirishaji, usindikaji, uhifadhi hadi kufikishwa mezani kuliwa unaangaziwa.

UN inaliona suala la usalama wa chakula na kuwapo lishe bora kwa kile kinacholiwa kuwa msingi wa kufanikisha Malengo 17 ya Maendeleo (SDGs), mojawapo ikiwa ni kuwezesha kila mtu kuwa salama.

Kimsingi, kinachoguswa hapa ni miongoni mwa malengo ya SGDs, hasa lile linaloangazia zaidi upande wa afya, ili kuhakikisha kila mtu anakuwa na afya bora.

Nasi tunakubaliana na mipango ya UN kwamba ipo haja ya kuhakikisha usalama katika chakula ili kulinda afya za Watanzania badala ya kuwapo mianya inayochangia baadhi ya watu kuhatarisha afya za wenzao.

Tunakubaliana na kile ambacho kinafanywa na UN, kwani kitasaidia watu kuzingatia afya kuanzia uzalishaji wa chakula, mazao shambani, mifugo, samaki, hadi usafirishaji, usindikaji, uhifadhi hadi kufikishwa mezani kuliwa.

Kwa nchini, kumekuwapo na taarifa kuwa, baadhi ya wakulima wakiwamo wa bustani hasa mboga, ambao hudaiwa kumwagilia maji ambayo si salama yakiwamo majitaka, hali ambayo ni hatari kwa afya za walaji.

Wakati hao wakifanya hivyo, hata waandaji wa vyakula vya kuuza wakiwamo mama lishe na baba lishe, nao hudaiwa kuweka hamira kwenye ugali ili wateja washibe kwa kiasi kidogo cha ugali.

Kwa upande mwingine, wauza supu na pweza, hudaiwa kuweka viagra, huku wale wanaokaanga chips wakidaiwa kutumia mafuta ya transfoma, lakini maziwa kuchanganywa na maji, unga wa ngano, ili kupata mtindi mzito.

Sisi tunaona ni wakati mwafaka kuwapo kwa mkutano, huo kwa ajili ya kusaidia dunia kutambua umuhimu wa ubora wa chakula na kuachana na mtindo huo tulioutaja ambao ni hatari kwa afya.

Kwa hapa nchini, tunashauri mamlaka kufuatilia kwa karibu taarifa za kuwapo kwa baadhi ya watu kuweka katika mazao au kuandaa vyakula katika mazingira hatarishi na kuchukua hatua za kisheria.

Tunaamini kwamba hatua zikichukuliwa, zikiwamo za kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa afya bora, usalama wa chakula utakuwapo kuanzia mashambani hadi nyumbani kinapoandaliwa hadi mezani kinapoliwa.

Hatua hiyo inaweza kusaidia wahusika kufanya shughuli zao kwa kuzingatia afya zao na za wateja wao kwa kuepuka kuweka hamira kwenye chakula, kuweka viagra au kukaangia mafuta ya transfoma.

Bila kufanya hivyo, afya za watu wengi zitakuwa hatarini na matokeo yake ni baadaye kuathiri nguvu kazi ya taifa pamoja na kuwa na taifa la watu wasiokuwa na mchango katika uzalishaji na uchumi kwa ujumla.

Tunashauri kwamba sisi kama taifa tusikubali watu wachache wenye maslahi binafsi kulifanyia mzaha suala la usalama wa chakula. Hivyo, Tanzania ikiwa mwanachama wa UN, ichukue hatua madhubuti za kuwalinda wananchi wake.

Habari Kubwa