Usawa wa jinsia utaletwa na ushirikiano wa pamoja

07Sep 2017
Mhariri
Nipashe
Usawa wa jinsia utaletwa na ushirikiano wa pamoja

KWA muda mrefu mashirika ya wanaharakati wa utetezi wa jinsia yamekuwa yakilalamikia kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia nchini kati ya wanawake na wanaume.

Mashirika hayo na wanaharakati binafsi wamekuwa wakisema kuwa wanawake wanafanyiwa vitendo vya ukatili, ubaguzi, udhalilishaji na unyanyapaa pamoja na kutokuwezeshwa hivyo kuwa waathirika wakubwa wa umaskini.

Baadhi ya vitendo ambavyo wamekuwa wakilalamikia ni kuwanyima wanawake na watoto wa kike fursa ya elimu, ajira, kumiliki na kurithi mali, kubakwa, kukeketwa, mimba za utotoni na ndoa za utotoni kwa kutaja baadhi.

Kutokana na hali hiyo, wamekuwa wakiinyooshea serikali kidole kwamba inahusika kwa namna mbalimbali kutokana na kutochukua hatua stahiki.

Kitu ambacho inaonekana wanaharakati hao hawakukiona ni suala la ushirikiano na nguvu ya pamoja katika suala zima la kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Jambo la kufurahisha ni kwamba Tamasha la 14 la Jinsia la mwaka 2017 linaloendelea jijini Dar es Salaam tangu juzi, lilibainisha umuhimu wa kuwapo kwa ushirikiano na nguvu ya pamoja miongoni mwa wadau na serikali.

Umuhimu wa ushirikiano na nguvu ya pamoja katika kuleta usawa wa kijinsia ulibainishwa na kusisitizwa na wazungumzaji siku ya uzinduzi wa tamasha hilo, linaloratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa mgeni rasmi, alibainisha umuhimu huo kwa kusema inahitajika nguvu ya pamoja kati ya serikali na mashirika katika kuleta usawa wa kijinsia na kuwaondolewa wanawake umaskini.

Samia alihimiza umuhimu wa kuzitafutia majibu sahihi changamoto zinazokwaza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na kuipongeza TGNP kwa kuacha kulalamika kama ilivyokuwa zamani na kuanza kuzitafutia majibu.

Mbali na Samia, wengine waliozungumzia umuhimu wa ushirikiano katika kuleta usawa wa kijinsia na kutekeleza kwa mafanikio Mpango wa Maendeleo Endelevu ni Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa Kitengo cha Wanawake, Hodan Addou; Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnitt na Balozi wa Ireland nchini, Fionnuala Gilsenan.

Ushauri wao ni muhimu sana, hivyo tunaamini kuwa washiriki wa jukwaa hilo, watauzingatia kwa kuibua changamoto mbalimbali zinazokwaza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na kupanga mikakati ya pamoja kwa ajili ya kukabiliana nazo.

Mikakati hiyo ikishawekwa hainabudi kutekelezwa kwa ushirikiano na kati ya wadau, serikali na washirika wa maendeleo, ili malengo ya kufikia maendeleo endelevu yafikiwe.

Kitu cha kujivunia ni ahadi ya serikali iliyotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Sihaba Nkinga, kwamba wizara itaendelea kuratibu juhudi za wadau ikiwamo kuandaa mpango wa kitaifa kuwakomboa wanawake, ambao ulianza Julai mwaka huu na kutekelezwa katika mikoa 23.

Jitihada nyingine zilizochukuliwa na serikali ni kuongeza nafasi za wanawake katika nafasi za uongozi, uanzishaji wa Benki ya Wanawake (TWB), kuanzishwa mfuko wa wanawake ambapo kila halmashauri inachangia asilimia tano ya mapato na uanzishwaji wa vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) na Vicoba.

Kimsingi, serikali imefanya jitihada nyingi za kuleta usawa wa kijinsia ikiwamo kutunga sheria na sera, hivyo ni wajibu wa wanawake kutumia Jukwaa la Jinsia kupitia utekelezaji wa mipango iliyoanzishwa na kuja na mikakati mingine ambayo itasaidia katika harakati za kuleta usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake.

Habari Kubwa