Ushauri wa Bashungwa wanawake, vijana kukopa taasisi rasmi ufanyiwe

06Aug 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ushauri wa Bashungwa wanawake, vijana kukopa taasisi rasmi ufanyiwe

MAKUNDI maalum ya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yamekuwa yakikumbana na vikwazo vingi katika kufanya shughuli zao za kujitafutia riziki.

Makundi haya yamekuwa yakiitwa ya watu waliosahaulika, kutokana na mazingira na changamoto yanazokumbana nazo, ikiwamo kupata mikopo.

Pamoja na vikwazo vingine vinavyowakwamisha kupata mikopo hiyo, lakini kubwa ni kutokuwa na dhamana kwa ajili ya kukopeshwa na benki pamoja na taasisi rasmi za kifedha.

Utaratibu uko wazi kuwa anayetaka kukopa benki au taasisi zingine rasmi za kifedha, ni lazima aweke dhamana hususan mali zisizohamishika kama nyumba, kiwanja, shamba nakadhalika, masharti ambayo ni magumu kwa wananchi wanyonge, yakiwamo makundi hayo.

Kwa kulitambua tatizo hilo, serikali ilijaribu kupunguza ukubwa wa tatizo hilo kwa kuziagiza halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya kuyakopesha makundi hayo kwa lengo la kuyawezesha kujikimu kimaisha kupitia shughuli za ujasiriamali.

Kwa mujibu wa maelekezo ya serikali, kila halmashauri inatakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuyakopesha makundi hayo, ingawa uzoefu umeonyesha kuwa upatikanaji wa fedha kwenye halmashauri nyingi ni changamoto.

Halmashauri nyingi zimekuwa zikilalamika kushindwa kutenga fedha za mfuko huo, ambapo sababu kubwa ni kuwa na vyanzo vichache vya mapato ya ndani pamoja na baadhi ya vyanzo vingine kuchukuliwa na Serikali Kuu.

Kutokana na hali hiyo makundi haya yanakwama kupata mikopo inayostahili, hivyo kupata kidogo, wakati mwingine hata hicho kidogo kuchelewa kukipata na wakati mwingine kukosa kabisa.

Njia iliyochukuliwa na wajasiriamali hao ni kujaribu kutafuta mikopo kwa njia zingine, ikiwamo kwa wakopeshaji binafsi ambao wametapakaa mitaani, huku wakiwakopesha wahitaji wa riba kubwa kupitiliza, ambazo mwishowe ni kuwafilisi wakopaji.

Serikali imeshaliona tatizo hilo ambalo limesababisha makundi ya wajasiriamali kukwama baada ya mali zao kufilisiwa na wakopeshaji kutokana na riba kubwa za marejesho ya mikopo.

Jana Waziri Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, aliwataka wajasiriamali wanawake na vijana kutohofia kuomba mikopo kwenye taasisi kubwa za fedha zikiwamo benki ili kujiepusha na mikopo isiyo rasmi ambayo imekuwa ikiwagharamu kwa kuwatoza riba kubwa, hivyo kuwarudisha nyuma kiuchumi.

Waziri Bashungwa alitoa wito huo wakati akifungua Kongamano la Biashara na Kilimo lililoandaliwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake na Vijana (TABWA) kwa kushirikiana na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwenye Viwanja vya Maonyesho ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye Uwanja wa Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu .

Waziri Bashungwa aliziomba pia taasisi za fedha nchini kusikiliza vilio vya wanawake na vijana, ambao wamekuwa wakilalamikia ugumu wa masharti yanayoambatana na mikopo hiyo, ambayo yanakuwa kikwazo kwao.

Kwa mujibu wa Bashungwa, licha ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya wanawake wenye ujasiri wa kubuni na kuendesha biashara, kasi ya ukuaji wa mitaji yao bado ni finyu, na kwamba inafahamisha dhahiri kuwa chanzo kikuu cha mitaji yao ni mikopo ya kibiashara, ila changamoto inabaki kuwa wengi wao hawana mikopo kutoka kwenye taasisi rasmi za kifedha na matokeo yake wanaangukia kwenye mikopo isiyo rasmi inayowanyonya sana kwa riba kubwa.

Alisema ndiyo maana ameziomba benki kubwa ziwasaidie pamoja na kuwaelimisha. Sisi tunaiona changamoto hii kuwa inahitaji mipango, mikakati na nguvu ya pamoja kwa ajili ya kukabiliana nayo. Jambo la msingi na la kupongeza ni wazo aliloliibua Waziri Bashungwa, hivyo kilichobaki ni wizara na taasisi za serikali kuketi pamoja kuangalia utekelezaji wake ili kuwakwamua wajasiriamali wetu wanawake na vijana.

Habari Kubwa