Ushauri wa mwenyekiti wa PAC ufanyiwe kazi

01Sep 2017
Mhariri
Nipashe
Ushauri wa mwenyekiti wa PAC ufanyiwe kazi

MATUMIZI mabaya ya fedha za umma yamekuwa yakibainika kila mwaka kutokana na ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Ripoti yake imekuwa ikiwekwa hadharani kila mwaka kwa ajili ya umma kujua pamoja na kuwasilishwa bungeni kisha wabunge kuijadili.

Ni ripoti ambayo imekuwa ikibainisha madudu ya matumizi ya fedha na rasilimali nyingine za umma katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa (Halmashauri), taasisi, mashirika, idara za serikali na wakala.

Jambo ambalo limekuwa likihojiwa ni serikali kutoifanyia kazi ripoti hiyo ya ukaguzi kuwashughulikia wahusika wa ufisadi huo, achilia mbali kutokuitumia kwa ajili ya kuziba mianya yote inayosababisha hali hiyo.

Kimsingi, ripoti ya CAG ni muhimu na ni chachu katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisdi ikiwa mamlaka zitaitumia kwa kuwa imesheheni taarifa na takwimu muhimu kuhusiana na usimamizi na matumizi ya rasilimali za umma.

Inajitosheleza kwa kuwa inaandaliwa baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa wataalamu waliobobea, hivyo mambo yanayobainishwa hayahitaji uchunguzi.

Kutokana na Tanzani kuwa miongoni mwa nchi zenye kiwango kikubwa cha rushwa, licha ya serikali ya awamu ya tano kuanza kwa kasi kubwa kuchukua hatua za kupambana nayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, amependekeza mambo matatu ambayo yakitekelezwa yanaweza kusaidia katika mapambano dhidi ya kansa hiyo.

Katika mahojiano mahususi na Nipashe ambayo tuliyachapisha kwenye toleo la jana, alisema njia ya kwanza ni kuhakikisha mikataba yote ya miradi ya serikali inapitia bungeni, ili ichambuliwe kwa kina kabla ya kupitishwa kwa kuwa usiri uliopo katika mikataba mikubwa ya serikali ndiyo umechangia kuwapo kwa ufisadi wa mali ya umma.

Kaboyoka anasema mikataba imekaa kiajabu sana na mkandarasi anaweza kubadili masharti ya mkataba kwa matakwa yake mwenyewe.

Njia ya pili ni kumwezesha CAG kifedha, ili akague miradi kiufanisi katikati ya utekelezaji wa miradi, ili kuona mwenendo mzima. Kwamba hatua hii italeta ufanisi tofauti na sasa ambapo CAG anakagua ambapo pesa imeshatumika vibaya na hana la kufanya bali kutoa hati chafu baada ya mwaka mzima huku PAC ikiishia kutoa tu mapendekezo kwenye Bunge juu ya hatua za kuchukuliwa.

Hatua ya tatu Mwenyekiti huyo anapendekeza umuhimu wa kuwapo chombo cha kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa na serikali hasa kwenye makosa yanayojirudiarudia, kungekuwa na uwazi zaidi, kwa kuwa kila kamati inafanya kivyake vyake na mapendekezo ya kamati hizo hakuna chombo kinachofanya ufuatiliaji.

Anapendekeza kuundwa kwa Kamati ya Bunge inayofuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya kamati zote, ili serikali iweze kuwajibishwa kwa uwazi zaidi.

Hatua anazozipendekeza Mwenyekiti huyo wa PAC zina mantiki na ni msaada mkubwa katika kudhibiti ufujaji, wizi na ubadhirifu wa fedha za umma.

Suala la kumwezesha CAG kifedha limekuwa likisisitizwa na wengi kutokana na kupewa fedha kidogo ambazo haziwezi kumwezesha kufanya ukaguzi maeneo yote, lakini pia ukaguzi wa miradi ukiendelea kutekelezwa ni muhimu kwa kuwa ni rahisi kuusitisha mradi husika itakapoonekana kuna ubadhirifu.

Pia kuwapo Kamati ya Bunge ya ufuatiliaji utekelezaji na mikataba kupitia bungeni ni hatua ambazo zitasaidia jitihada za kudhibiti ufisadi.

Bila shaka serikali imeusikia ushauri wa Mwenyekiti huyo wa PAC na utafanyiwa kazi. Wito wetu ni kwa watu wengine wenye nia ya dhati ya kudhibiti ufisadi nchini wanajitokeza kutoa ushauri wa nini kifanyika katika kufanikisha vita hii.

Habari Kubwa