Usimamiaji makini wa migodi utaongeza mapato

03Aug 2017
Mhariri
Dar es salaam
Nipashe
Usimamiaji makini wa migodi utaongeza mapato

JITIHADA za serikali ya awamu ya tano za kuhakikisha Watanzania na taifa kwa ujumla wananufaika kwa rasilimali zilizoko nchini, zimeendelea kuzaa matunda, baada ya kuongezeka kwa mapato ya serikali kutokana na mrabaha.

Mafanikio hayo yametokana na kutumika kwa sheria mpya ya madini. Safari hii, serikali imepata Sh. milioni 334 za mrabaha kwa kipindi cha mwezi mmoja kupitia mgodi wa kuchenjua dhahabu wa Sunshine uliopo Chunya, mkoani Mbeya.

Imeelezwa fedha hizo zimetokana na ongezeko la mrabaha lililotangazwa mwezi uliopita na Wizara ya Nishati na Madini, kutoka asilimia nne hadi sita.

Ofisa Madini wa Mkoa wa Mbeya, Said Mkwawa, alibainisha mafanikio hayo juzi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipotembelea mgodi huo, ambao unachenjua dhahabu kwa asilimia 99 ya madini.

Mkwawa alifafanua kabla ya kupitishwa kwa sheria hiyo mpya, serikali ilikuwa inapata mrabaha wa Sh. milioni 191 kwa kilogramu 55,562 zinazozalishwa na mgodi huo kila mwezi.

Ongezeko la mapato yatokanayo na mrabaha ni mafanikio makubwa kwa taifa kwa sababu yataiongezea serikali uwezo wa kujiendesha sambamba na kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ikisuasua kutokana na ukosefu wa bajeti ya kutosha.

Kwa muda mrefu nchi yetu ilipoteza mapato yake makubwa katika sekta ya madini, kutokana na mambo mbalimbali na matokeo yake mapato yatokanayo na rasilimali ya madini kuwanufaisha wawekezaji huku wananchi wakibaki katika umaskini.

Tunaweza kusema miongoni mwa mambo yaliyochangia nchi kutonufaika na mapato ya madini ni kukosekana kwa uwazi na sheria nzuri ambazo zingehakikisha nchi inanufaika sambamba na kuziba mianya yote ya kuwafanya baadhi ya wawekezaji kutorosha rasilimali hiyo.

Kukosekana kwa uzalendo na uadilifu pia ni sababu iliyochangia hali hiyo, kwa kuwa baadhi ya watumishi wa umma waliopewa dhamana ya kusimamia madini hawakutimiza wajibu wao.

Kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuhusu makinikia ya dhahabu mwaka huu zilibainisha jinsi watumishi hao walivyohusika katika hujuma hizo huku baadhi ya majina yao yakiwekwa hadharani.

Ripoti yao iliweka wazi tangu uwekezaji katika migodi nchini ulipoanza mwishoni mwa miaka ya tisini, Tanzania imepoteza kiasi kikubwa cha fedha Sh. trilioni 425. Kiasi hiki ni kikubwa kiasi kwamba zingeweza kuwa bajeti ya taifa kwa takribani miaka 14.

Ongezeko la asilimia mbili kutoka nne hadi sita katika mrabaha, limebainisha ongezeko kubwa la mapato ya serikali na pengine kama asilimia hiyo ingekuwa inatozwa tangu miaka ya nyuma, taifa letu lingekuwa limevuna fedha nyingi ambazo zingesaidia kulipaisha kiuchumi.

Uamuzi wa kuanza utekelezaji wa sheria mpya ya mrabaha ya kuongeza asilimia ya tozo umetupatia somo kuwa sekta ya madini inalipa, isipokuwa jambo la msingi ni kuwapo kwa usimamiaji wa karibu na makini wa migodi yetu, ambao utawezesha kuwapo kwa ongezeko zaidi la mapato.

Somo tulilopata kutoka mgodi wa Sunshine linapaswa kuiamsha usingizini serikali ili iwe makini katika kufuatilia kodi ya mrabaha katika migodi yote nchini.

Katika kufanikisha lengo la kukusanya mapato zaidi kutoka katika madini, tunaishauri Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inaweka utaratibu mzuri wa kuwafuatilia watendaji wake wa ofisi za madini wanatekeleza majukumu yao kwa uzalendo, uwazi, uaminifu, uadilifu na kwa uwajibikaji mkubwa.

Kwa kufanya hivyo, Taifa litaongeza mapato kutoka katika sekta ya madini, hivyo kuelekezwa katika utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo ambayo itabadili maisha ya wananchi.

Habari Kubwa