Ustawi wa sekta ya michezo unahitaji viongozi wabunifu

27Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ustawi wa sekta ya michezo unahitaji viongozi wabunifu

KUNA tatizo kubwa katika sekta ya michezo nchini. Moja ya kiini cha kukwamisha ustawi wa sekta hiyo ni uwapo wa viongozi wabovu na wasiokwenda sambamba na mahitaji ya sasa.

Viongozi wetu katika sekta ya michezo wameshindwa kufikia malengo ya mafanikio kutokana, aidha kukosa ubunifu, kujituma au uwezo mdogo wa kuongoza usiokuwa na upeo wa kile kinachohitajika.

Viongozi wetu wameifanya michezo kuwa sehemu ya kujinufaisha, hawajabeba dhamana ya kuifanya michezo kama alama ya maendeleo kwa jamii.

Ndiyo maana, kwenye mambo yanayohitaji utaalamu, viongozi wetu wa michezo wanaingiza masuala ya siasa. Hili ni tatizo kubwa tunapozungumzia ustawi wa sekta ya michezo.

Viongozi wetu wameshindwa kuwa wabunifu, hakuna uwekezaji wa kutosha katika sekta hii licha ya kuwapo kwa fursa nyingi. Hakuna uwekezaji wenye dhamira ya dhati kuinua michezo kuanzia ngazi za kijiji hadi Taifa, ambako ndiko kwenye kiini cha vijana wengi wenye vipaji.

Lakini pia kukosekana kwa wataalamu wa kuibua vipaji ni moja ya sababu nyingine inayokwamisha nafasi ya wachezaji chipukizi kupata fursa ya kung’ara. Hata pale wataalamu wa michezo wanapofika nchini, hawapewi fursa ya kutembelea maeneo yote ya nchi yetu kwa ajili ya kusaka vipaji.

Nipashe kama wadau wa michezo, tungependa kuona sekta hiyo inajikomboa kutoka katika utumwa wa ubabaishaji hadi kwenye nafasi ya maendeleo.

Tunasema hayo tukiamini, jukumu la mageuzi haya liko ndani ya uwezo wetu kama kweli tutasutwa na ukosefu wa dhamira ya dhati kufanya mabadiliko.

Tungependa kuona viongozi katika sekta ya michezo kuanzia ngazi za chini hadi taifa wanatimiza wajibu wao wa kuinua sekta hii badala ya kujali na kutanguliza mbele maslahi yao binafsi.

Ni kichekesho kudhani kuwa, michezo nchini inaweza kufikia kiwango cha maendeleo kwa kutegemea ufadhili kutoka nje pekee.

Dunia ya sasa inamweka mbali na mafanikio mtu asiyetaka kwenda sambamba na mabadiliko yanayotokea kila uchao.
Kama wanamichezo, tusingependa kuwa sehemu ya kundi la watu wasioguswa na mabadiliko ya lazima katika kuinua michezo.

Wadau wangependa kuiona sekta hiyo ikiwa ni fursa muhimu ya kuzalisha ajira na kuingiza pato kubwa kwa serikali. Michezo isiwe sehemu ya burudani peke yake, bali pia iwe chanzo kikuu cha mapato ya serikali.

Katika kufikia malengo hayo, ni lazima wadau wakubali kufanya mageuzi makubwa ya viongozi wa michezo. Ni wakati wa kubadilika na kuachana na utamaduni wa kuchagua viongozi kwa kigezo cha kujuana badala ya kuzingatia uwezo, uzoefu, utendaji na weledi wa mtu.

Huu siyo tena wakati wa kuwaweka madarakani viongozi kwa sababu ya uswahiba, undugu, urafiki au ujirani. Tunahitaji kuchagua viongozi wenye mtazamo mpya, wenye mwelekeo wa kutaka mabadiliko kila uchao na wabunifu.

Kuendelea kuwa na viongozi waliofika mwisho wa upeo wa kufikiria kuleta maendeleo, maana yake ni kunyima fursa za uwekezaji kuanzia ngazi za chini, ambako ndiko kwenye hazina ya vipaji.

Tisipofanya hivyo, tutaendelea kuwa ni watu wa shindwa na kubakia kulalamika wakati wenzetu wakisonga mbele.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa