Utalii wa fukwe ni muhimu, zirudi Maliasili na Utalii

26Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Utalii wa fukwe ni muhimu, zirudi Maliasili na Utalii

JUZI Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Leila Muhamed Mussa, alitembelea vyombo vya habari vya IPP Media, na kueleza mikakati ya kukuza na kuendeleza utalii visiwani Zanzibar ambavyo uchumi wake unategemea biashara ya utalii kwa asilimia 28.

Baadhi ya mikakati ni kuibua vivutio vipya ikiwamo kuendeleza utalii wa majengo ya kale na utamaduni kwa kutumia wananchi wa eneo husika kupokea na kutembeza wageni.

Licha ya kuwapo kwa janga la virusi vya homa kali ya mapafu (corona), na kusababisha ugonjwa wa Covid-19, lakini jitihada mbalimbali zimefanyika kuhakikisha watalii wanaendelea kuja nchini na kwa sasa visiwa hivyo vinapokea watalii kutoka Ulaya Mashariki ambako hakujaathiriwa sana na corona.

Tunaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mpango huo wa kubuni, kuendeleza na kuboresha vivutio vya utalii, kwa kuwa sasa mtalii atakuwa na kila sababu ya kurudi kwa kuwa hakupata nafasi ya kuvimaliza alivyokuja nchini.

Tanzania imebarikiwa hifadhi za taifa 22, mapori ya akiba 32, mapori tengefu 18, Jumuiya ya Uhifadhi za Jamii (WMA), Mamlaka ya Hifadhi Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Maeneo ya mtawanyiko, shoroba za wazi, ambayo yote ni muhimu kwa uhifadhi.

Mara nyingi katika kila kivutio kuna bidhaa tofauti zinazouzwa kulingana na mahitaji ya mgeni, na sasa kumekuwa na jitihada za kuleta bidhaa mpya hasa baada ya kuwapo kwa janga la corona ili kumhakikishia mgeni furaha.

Mathalani, Ngorongoro wameanzisha utalii wa miamba na sura ya nchi ambayo mtalii anaweza kutembelea maeneo mbalimbali kwa safari za miguu, kujionea uumbaji wa miamba huku akiona wanyama.

Lakini Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), imekuja na bidhaa mpya za kucheza na samaki maalum kwa watalii ambao ni wanamichezo hupenda kumuona kwa jinsi alivyo mtundu, lakini mtalii anaweza kufanya safari ya kutembea umbali fulani na kulala kwenye mahema maalum au kwenda na kurudi.

Yote yanafanyika kama mbinu ya kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali nchini, lakini kuondokana na utalii wa mazoea kwamba utaenda kuona wanyama ukiwa ndani ya gari basi, lakini ikiwa mtalii atapika na kula chakula porini atajiona kaishi maisha ya tofauti na kuona kweli ametalii na kufurahia, ikiwamo kuongeza siku za kukaa nchini.

Waziri huyo alieleza kuwa Zanzibar imejipanga kuongeza vivutio vya utalii ili mtalii aweze kuwa na maeneo mengi zaidi ya kutembelea, jambo ambalo litaongeza siku za kuishi nchini na fedha atakazotumia, lakini itamlazimu kupanga safari nyingine ya kurudi kuona vile ambavyo hakuviona awali.

Katika kuongeza vivutio vya utalii hapa ndipo serikali inapaswa kuangalia kwa jicho la pekee utalii wa fukwe ambao haujatumika, mathalani Zanzibar ina fukwe nzuri, kubwa na zenye kusifiwa duniani, lakini bado hazijaendelezwa na kutumika vyema, ikiwa nguvu kubwa itawekezwa huko maana yake idadi ya vivutio itaongezeka.

Pia Tanzania kuna fukwe nzuri na kubwa kuanzia Tanga hadi Mtwara, lakini zipo chini ya Wizara ya Uvuvi, jambo ambalo linasababisha ziwe ni kwa ajili ya uvuvi pekee, lakini hazitumiki kwa ajili ya watu kutalii na kuliingizia taifa fedha za kigeni.

Unapotembelea mji wa Durban, Afrika Kusini utaona jinsi fukwe zilivyojengwa kisasa na mamia ya watalii wa ndani na nje humiminika kutalii huku wengine wakifanya michezo mbalimbali ya kwenye maji kwa kutumia vifaa maalum. Kama huko imewezekana, maana yake fukwe za Tanzania zina nafasi kubwa ya kutumika kwenye utalii.

Habari Kubwa