Utaratibu mpya wa kupata majaji utasaidia

20Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Utaratibu mpya wa kupata majaji utasaidia

SERIKALI imebadili mfumo wa kupata majaji ya Mahakama Kuu ya Tanzania na kuanzia sasa ajira yao itakuwa inashindanishwa katika hatua ya awali, badala ya kuwa ya uteuzi wa moja kwa moja wa rais.

Mabadiliko ya utaratibu huo mpya yalitangazwa juzi kupitia tangazo la Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo ipo chini ya Jaji Mkuu, ikiwataka watu wenye sifa kuwasilisha barua za maombi kabla ya Agosti mosi.

Miongoni mwa sifa zinazohitajika ni shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu kinachotambulika na mamlaka udhibiti Tanzania na muombaji awe aliwahi kuwa hakimu miongoni mwa sifa nyingine na vile vile kuwahi kufanya kazi katika utumishi wa umma kama wakili au wakili wa kujitegemea.

Zingine ni kusajiliwa kuwa wakili, na kuwa na sifa hizo mfululizo kwa muda usiopungua miaka 10.

Hata hivyo, utaratibu huo mpya hauwahusu watumishi wa makahakama kwa kuwa wana utaratibu mahsusi wa ndani.

Pamoja na kuwa utaratibu huo hautamzuia rais asiteue mtu yeyote anayemuona anafaa, lakini tunaona kuwa utaongeza wigo wa uteuzi badala ya kuwategemea walioteuliwa na rais peke yao na pia watakuwa watu wenye sifa zainazotakiwa sambamba na kuweka uwazi utakaopunguza malalamiko, kwa kuwa watakaopatikana watakuwa wamepitia mchujo.

Kumekuwapo na malalamiko kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiteuliwa kuwa majaji bila kuwa na sifa za kutosha kutumikia nafasi nyeti ya kutoa maamuzi ya kesi.

Kupitia utaratibu huo mpya, mahakama itawapata majaji ambao ni wabobezi katika taaluma ya sheria kwa kuzingatia kwamba kwa sasa dunia inabadilika kwa kasi na changamoto zinaongezeka kila uchao.

Pamoja na utaratibu mpya kupanua wigo katika uteuzi wa majaji, tunaona kwamba kuna haja ya kuliweka suala hilo katika katiba ili liwe la kisheria badala ya kuendelea kumwachia rais utashi wa kuteua majaji anaowataka.

Tunasema hivyo kwa kuwa suala hilo bila kuwa la kikatiba, yanaweza kutokea mazingira ya kukwamisha utekelezaji wake au kutokea mgongano katika upatikanaji wa majaji.

Kwa kuwa rais amepewa mamlaka kubwa ya kuteua, itakuwa vizuri kumpunguzia majukumu angalao ya uteuzi wa watendaji wa mhimili wa mahakama, lengo likiwa ni kuwa na majaji ambao watatoa maamuzi kwa uhuru na yasiyoacha shaka yoyote kwa watu wote watakaokwenda mahakamani kutafuta haki.

Suala la uteuzi wa majaji kufanywa na Tume ya Utumishi wa Mahakama ni miongoni mwa mapendekezo yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba mpya iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uwenyekiti wa Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba.

Katika Katiba ya Kenya iliyoandikwa baada ya maridhiano, suala hilo liliingizwa na kuweka wazi kwamba nafasi za ujaji ni za kuomba na kufanyiwa usaili ikiwamo ya jaji mkuu ambayo kwa sasa inashikiliwa na Dk. Willy Mutunga, aliyeomba na kuteuliwa.

Tunashauri pia kwamba iko haja ya kupanua wigo katika uteuzi wa nafasi zingine kwa kuzipa mamlaka baadhi ya taasisi kufanya kazi hiyo kwa kuzitangaza nafasi ili watu wenye sifa waziombe badala kusubiri uteuzi. Faida yake ni kwamba wanaozipata nafasi hizo wanakuwa ni watu wenye uwezo, uzoefu na wanaoweza kuleta matokeo chanya.

Jambo hilo linawezekana kama lilivyowezekana Kenya na tunaamini kuwa likitekelezwa, utekelezaji wa shughuli za serikali utakuwa wa tija na ufanisi.

Habari Kubwa