Utaratibu wa chanjo uwe wazi na shirikishi

23Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Utaratibu wa chanjo uwe wazi na shirikishi

JANA Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema chanjo zimefika nchini na anayehitaji kuchanjwa yupo huru kuchanjwa wakati wowote, katika vituo maalum vilivyopangwa kwa huduma hiyo.

Aidha, amesema serikali ilichukua uamuzi wa busara wa kuagiza na kuziletea chanjo nchini baada kugundua kuna Watanzania ambao ni wafanyabiashara na wasafiri wa shughuli tofauti nje ya nchi, ambazo sharti upatiwe au kuwa na cheti cha chanjo kuingia nchini mwao.

Pia, serikali ilisema kuna chanjo mbili ambazo zimepitishwa kwa Watanzania kutumia. Hii ni taarifa nzuri kwa umma kwa kuwa sasa wale wanaotaka kuchanja watapata huduma hiyo kwa wakati muafaka.

Ni muhimu sasa serikali iweke wazi hospitali maalum za kutoa chanjo hiyo kwa kuwa wanaotaka kuchanja ni wengi wanasubiri kujua ni wapi pa kwenda, ili kupata huduma hiyo.

Lakini taarifa ni nyingi kuwa ili uchanjwe ni lazima upimwe corona, kama huna ndiyo uchanjwe, kuliko kuchanjwa ukiwa na maradhi hayo mwilini athari zake ni kubwa na husababisha hata watu kupoteza maisha.

Pia, umuhimu wa chanjo kwa kuwa zipo taarifa kuwa ikiwa umechanjwa na unachangamana na wasiochanjwa kuna uwezekano wa kupata maambukizi, huku wengine wakidaiwa kupoteza maisha baada ya kupata chanjo, na wengine wakibaki na athari mbalimbali jambo linaloogopesha watu kufanya uamuzi.

Zipo taarifa kuwa baadhi ya watu huenda wakapoteza maisha, na kuna waliopoteza maisha baada ya kuchanjwa, hizi zote ni taarifa zinazopaswa kuwekwa vizuri kwa umma ili kuwe na uelewa wa kutosha.

Lakini ni muhimu chanjo zikatajwa ili kuondoa minong’ono kuhusu chanjo zinazotumika nchi mbalimbali duniani au zilizoaanza kutumiwa kwenye ofisi za kimataifa nchini.

Suala la chanjo limekuwa na maneno mengi huku kukiwa na taarifa nyingi duniani baadhi ya nchi zikisema hazitakubali waliopata chanjo za nchi fulani kuingia nchini mwao, hali inayowalazimu waliochanjwa chanjo ilisiyokubaliwa na nchi nyingine basi wachanjwe kwa kadri ya matakwa.

Tunajua serikali ilituhakikishia kuwa itafanya utafiti wa chanjo kabla ya kukubali ipi inayofaa kutumika nchini, na kuwataka wananchi kuwa watulivu huku mipango ya kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo ikiendelea.

Taarifa zote hizi ni muhimu zikawafikia wananchi na kwa kuwa kuna mpangilio kwenye mamlaka za serikali za mitaa, ni rahisi kufikisha ujumbe kwa umma ili waweze kufanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi kwa manufaa yao.

Ni muhimu elimu hii ikaanzia ngazi ya mtaa, kijiji, kata, tarafa na wilaya kupitia mikutano muhimu ambayo huleta pamoja wananchi, lakini kuwa na mabango yenye ujumbe wa kuelimisha umma lengo ni kuzishinda habari zinazovuma ambazo nyingine siyo za kweli.

Elimu sahihi itawezesha wananchi kupata chanjo kwa wingi kwa kuwa hakuna ubishi kuwa hali ilikofika ni lazima watu kupata chanjo.

Lakini kwa kuwa ni mara ya kwanza inatolewa nchini na inajulikana ni bure basi uwapo utaratibu mzuri kwenye hizo hospitali ili kusije kukazua majanga au kuongeza maambukizi ya ugonjwa huo wakati ingewezekana kuzuia.

Pia, ni muhimu elimu kwa umma ikaendelea kutolewa kwa wingi namna ya kujikinga kwa kuwa bado wananchi wengi hawafuati taratibu za kujikinga na corona, kuanzia kwenye vyombo vya usafiri wa umma, kwenye mikusanyiko na kwingine kokote.

Pia, ni muhimu kuelimisha umma umuhimu wa kufanya mazoezi asubuhi na jioni kwa kuwa ni namna sahihi ya kukabiliana na maradhi hayo.

Habari Kubwa