Utaratibu wa serikali kutumia kilichokusanywa utatuvusha

26Feb 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Utaratibu wa serikali kutumia kilichokusanywa utatuvusha

SERIKALI ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imeamua kutumia mfumo wa ‘Cash Budget (kutumia kilichokusanywa).

Lengo la kutumia kilichokusanywa ni kuweka nidhamu katika matumizi ya fedha za umma sambamba na fedha za makusanyo kutoka vyanzo mbalimbali kuelekezwa katika maeneo ya vipaumbele.

Wizara ya Fedha na Mipango imesema kuwa mfumo wa kupanga na kutumia kinachokusanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), ndiyo ulioamuliwa kutumiwa na serikali ya awamu ya tano.

Mfumo huo ulitumiwa na serikali ya zilizopita baada ya mashauriano na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), lakini utekelezaji wake haukuwa endelevu.

Wizara hiyo inasema utaratibu wa huo utaendelea kutumika kila mwezi na kwamba kila makusanyo yatakayopatikana kwa mwezi husika, yatatumika kulingana na mahitaji husika ya mwezi huo.

Utaratibu wa serikali kupanga matumizi kulingana na makusanyo, ulitekelezwa na serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa na kwa kiasi kikubwa ulichangia kurejesha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.

Aidha, uliisaidia Serikali ya Mkapa kuelekeza fedha za makusanyo kwenye maeneo yaliyokuwa ya vipaumbele vya serikali yake ikiwamo kuanzisha na kuupatia fedha Mfuko wa Barabara pamoja na kulipa madeni ya nje. Ulipaji wa madeni hayo uliwarejeshea imani wahisani na kuamua kuifutia Tanzania madeni kupitia mpango wa kuzifutia madeni kundi la nchi 38 maskini zilizokuwa zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni (Hipic).

Bila shaka serikali imeamua kuutekeleza utaratibu huo kwa lengo la kuhakikisha kwamba serikali inakusanya na kutumia ilichokikusanya, hatua ambayo inadhibiti natumizi ya ovyo hata kama serikali haikukusanya.

Sisi tunaona kwamba utaratibu huo ni mzuri na utakuwa na tija kwa kuwa utawadhibiti watendaji waliokuwa wakizitumia fedha za umma kwa mambo yasiyo na tija huku mambo ya msingi hususan miradi ya maendeleo ikikosa fedha na kukwama.

Serikali imeshasema kuwa malengo ya makusanyo kwa Februari ni Sh. trilioni 1.03 na kuwa kwa mwezi huo imetumia zaidi ya Sh. trilioni moja katika miradi na sekta mbalimbali.

Shilingi bilioni 18.7 zimepelekwa kutekeleza mpango wa elimu bure, Sh. bilioni 1.65 mafunzo kwa vitendo katika vyuo 35, Sh. milioni 29.1 kununulia vifaa, Sh. milioni 1.49 zilitumika kulipa posho, Sh. milioni 402.1 zilitumika kulipia posho kwa wanafunzi. Sh. bilioni 573.2 zilitumika kulipa mishahara kwa watumishi wa umma, bilioni 842.1 zililipa deni la taifa, Sh.

bilioni 81.23 kulipa deni la mifuko ya hifadhi ya jamii, Sh. bilioni 166.1 zilitumika katika miradi ya maendeleo, Sh. bilioni 2.078 zilipelekwa Mamlaka ya Elimu Tanzania.

Kadhalika, Sh. bilioni 7.115 katika sekta ya maji na Sh. bilioni 58.168 sekta ya barabara, Sh. bilioni 40.73 sekta ya ujenzi na Sh. bilioni 16.46 zilipelekwa Tamisemi, Sh. bilioni 20.1 sekta ya umeme, Sh. bilioni 2.034 sekta ya reli na Sh. bilioni 12.3 Mahakama ya Tanzania.

Matumizi hayo yanaonyesha jinsi gani serikali ya awamu ya tano ilivyo makini na imedhamiria kuhakikisha fedha za walipakodi zinatumika kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Tunatambua kuwa utaratibu wa matumizi kulingana na makusanyo, una changamoto zake kama baadhi ya wachumi wanavyotoa angalizo kwamba ukusanyaji ukisuasua kila kitu kinasimama, kuwapo haja ya kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi bila kuidhoofisha sekta binafsi, lakini tunaamini kuwa utaipaisha nchi yetu kimaendeleo.

Habari Kubwa