Utatili kijinsia upingwe

11Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Utatili kijinsia upingwe

MAADHIMISHO ya siku 16 za kupinga ukatili zilifika kilele chake jana, kwa maeneo mbalimbali kuadhimisha kwa kuwa na maandamano, visa mkasa vya wanawake na wanaume waliopitia ukatili huo katika safari za maisha.

Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa ‘kizazi chenye Usawa: Simama Dhidi ya Ubakaji’, lengo ni kuongeza ushawishi, kubadilishana taarifa, uzoefu kujenga uwezo wa pamoja kwa jamii kupambana na ukatili wowote unaotokea kwneye jamii.

Chimbuko la siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni mauaji ya kinyama ya wadada wa Mirabelle yaliyofanyika nchini Dominika mwaka1960, mnamo mwaka 1991, Umoja wa Mataifa tarehe hiyo ukaifanya kuwa siku ya Kimataifa ya kupinga unyanyasaji dhidi ya wanawake.

Kwa makusudi hayo Umoja wa Mataifa ulitenga siku 16 ikiwa ni Novemba 25 ambayo ni siku ya tamko kupinga unyanyasaji dhidi ya wanawake na Desemba 10 ambayo ni siku ya Tamko rasmi la Haki za Binadamu ikiwa ni ishara ya kuhusisha ukatili huo na uvunjaji wa haki za binadamu.

Kwa Tanzania, jitihada zimefanyika ikiwamo kuruhusu mashirika yasiyo ya kiserikali kama Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Mashirika ya Umoja wa Mataifa UNFPA na UN- Women bara na visiwani, ambao kwa pamoja wametoa elimu kwa jamii na uragibishi kuhusu kupinga ukatili.

Aidha, jitihada nyingi kwa kushirikiana na wafadhili zimewezesha kuanzisha madawati ya jinsia kwenye vituo mbalimbali vya polisi ambayo yamewawezesha watu wote kutoa taarifa za ukatili wowote waliofanyiwa kwenye jamii.

Ukatili unaotendwa kwa jamii kwa kiasi kikubwa ni ndoa za utotoni ambazo ziliwafanya wasichana wengi wasiendelee na masomo.

Mwingine ni wanawake kunyimwa umiliki wa ardhi licha ya mabadiliko ya sheria ya ardhi kuruhusu, lakini mila na tamaduni za baadhi ya maeneo zimetumika kumnyima haki hiyo na kuendeleza mfumo dume.

Pia wa majumbani kwa maana ya ubakaji, ulawiti, vipigo kwa wanawake na wakati mwingine wahusika kutokutoa taarifa kwa kuogopa kuharibu mahusiano na wengine kuondoa kesi kwenye vyombo vya sheria.

Katika maadhimisho hayo kilio kikubwa kilikuwa madawati vya jinsia mbavyo baadh yameshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Kadhalika kwa vyombo vya sheria kwamba licha ya kuwapo ushahidi wote, lakini kesi zinachukua muda mrefu kiasi cha walioumizwa kukata tamaa na wengine kutofika mahakamani.

Pia, baadhi ya madaktari wametajwa kuharibu ushahidi kwa kuwa wanapewa rushwa ambayo huleta madhara kwenye kesi kama hizo hususan ikiwa aliyetenda jambo hilo ni mtu mwenye uwezo, na wakati mwingine jambo kumalizika au kuishia Polisi kwa madai ya kukosekana ushahidi.

Wakati wa maadhimisho hayo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, alitoa takwimu za miezi kumi zilioonyesha matukio ya ubakaji yameongezeka kutoka 608 hadi 719 kwa miaka mwili.

Takwimu hizi ni kiashiria bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuanzia kwenye jamii, wadau na taifa kwa ujumla kwa kuwa idadi ya watoto wanaobakwa yanaongezeka kwa kasi na waathirika ni watoto ambao hawawezi kujitetea.

Kuwapo kwa matukio haya maana yake jamii haijatimiza wajibu wake ipasavyo, na inapaswa kuchukua hatua kuanzia sasa kwa kuwa madhara ya kisaikolojia, kimwili kwa maana ya kuambukizwa maradhi mbalimbali ukiwmao Ukimwi ni mkubwa sana.

Ni rai yetu kwa serikali kuendelea kuimarisha madawati ya jinsia na ushirikiano thabiti kwa mashirika ambayo yanatoa elimu, uragibishi na jitihada mbalimbali za kuielimisha jamii kuondokana na fikra potofu ambazo zinazidi kumkandamiza mtoto wa kike na mwanamke kwa ujumla.

Habari Kubwa